VIDEO: Wabrazil Simba SC wajipigia chapuo

Dar es Salaam. Wakati Simba imeondoka leo kwenda Afrika Kusini kuweka kambi, mabeki wawili raia wa Brazil wametamba kuifanyia makubwa klabu hiyo.

Simba imewasajili Wabrazil watatu mabeki Tairone Santos Da Silva, Gerson Fraga Vieira na mshambuliaji Henrique Da Silva kwa mkataba wa miaka miwili kila mmoja.

Wakizungumza Dar es Salaam jana, Vieira ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo mkabaji, alisema ujio wake Simba ni kuendeleza mafanikio.

Vieira alisema hana wasiwasi juu ya ubora wake uwanjani kwa kuwa ana uwezo mzuri, hivyo akishirikiana na mabeki waliopo Simba itakuwa na ngome imara.

“Malengo yangu ni kucheza kwa juhudi, jambo la msingi ni kuwa na umoja na wenzangu ambao tutakuwa nao, kama beki najua majukumu yangu vyema Simba ni klabu ya mafanikio tunatakiwa kuendeleza kwa muda nitakaokuwa hapa,”alisema Vieira ambaye ndiye anajua lugha ya Kiingereza kuliko wenzake.

“Mpira hauna tofauti muhimu ni kujua kocha anataka kipi nifanye hivyo ili Simba ipate mafanikio, nafikiri tutakuwa na timu imara kwa msimu ujao kwa jinsi ninavyoona mpaka sasa.”

Tairone alisema ana uwezo wa kucheza mipira ya juu kwa kutumia hesabu. Tairone ambaye ana urefu wa mita 1.91 alisema urefu wake umekuwa silaha kubwa katika kukabiliana na mipira ya juu kwa kuzuia au kufunga.

“Unaona urefu wangu ni kitu kinachonisaidia kukabiliana na mipira ya juu kuhakikisha napiga kwa kuokoa na hata ninapopandisha mashambulizi pia naweza kufunga,”alisema Tairone.

Naye Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori alisema Simba itaweka kambi ya maandalizi ya wiki mbili kujiandaa kwa msimu mpya.

“Tukiwa Afrika Kusini timu itapata maandalizi ya msimu mpya tutakuwa huko kwa wiki mbili na baada ya muda huo tutarejea kwa mchezo wa Siku ya Simba, kila kitu kimekamilika katika safari yetu ya huko,”alisema Magori. Pia alisema beki Mganda Juuko Murshid ni mtoro na atachukuliwa hatua.