Waarabu waitega Simba

Muktasari:

  • Simba ambayo Jumamosi iliyopita ilipoteza mechi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inalazimika kupata matokeo mazuri katika michezo mitatu dhidi ya timu hizo kutoka mataifa ya Kaskazini mwa Afrika ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.

Dar es Salaam. Mechi tatu mfululizo zijazo dhidi ya Al Ahly na JS Saoura, zinaiweka Simba kwenye mazingira magumu ya kufuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Wawakilishi hao wa Tanzania wanapaswa kufanya kazi ya ziada kupata idadi kubwa ya pointi katika mechi hizo tatu, vinginevyo ndoto ya kusonga mbele itafutika rasmi.

Simba ambayo Jumamosi iliyopita ilipoteza mechi dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), inalazimika kupata matokeo mazuri katika michezo mitatu dhidi ya timu hizo kutoka mataifa ya Kaskazini mwa Afrika ili kuweka hai matumaini ya kusonga mbele.

Presha ya Simba baada ya kufungwa na AS Vita, ubora na uzoefu wa kikosi cha Al Ahly na kiwango cha kuvutia ndani ya uwanja ambacho timu kutoka ukanda huo zimekuwa nacho zinapocheza nyumbani, zinaipa mtihani mkubwa Simba kuandika rekodi ya kufika hatua ya robo fainali.

Ni lazima Simba ichange vyema karata zake na kuhakikisha angalau inavuna pointi kadhaa kwenye mechi hizo tatu vinginevyo hadithi yao katika hatua ya makundi itakamilika kabla hata ya kumaliza idadi yote ya michezo sita.

Baada ya mchezo wa ugenini dhidi ya AS Vita, Simba itasafiri tena hadi ugenini mjini Cairo, Misri ambako itacheza na Al Ahly, Februari 2 na baada ya hapo itarejea nchini kurudiana na waarabu hao siku 10 baadaye Februari 12.

Al Ahly imekuwa na rekodi nzuri ya kufanya vyema katika mechi za nyumbani na kwa misimu miwili mfululizo haijapoteza mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wakiwa kwao Misri.

Lakini pia timu hiyo inaundwa na kundi kubwa la wachezaji bora na wenye uzoefu ambao wamekuwa wakifahamu fika kutumia vyema makosa binafsi ya timu pinzani kufunga mabao.

Timu hiyo kwa sasa inaongoza Kundi D ikiwa na pointi nne, baada ya kuifunga AS Vita katika mechi ya kwanza na kutoka sare ugenini na AJ Saoura na ushindi wa mechi zake mbili dhidi ya Simba utaifanya kufikisha pointi 10 ambazo zinaweza kuwapa fursa ya kufuzu mapema hatua ya robo fainali.

Al Ahly haitabiriki na inaweza kuchukua pointi hata ugenini na mfano ni matokeo ya sare ya bao 1-1 iliyopata dhidi ya AJ Saoura mwishoni mwa wiki iliyopita.

Simba ikimalizana na Al Ahly katika mechi hizo mbili za ugenini na nyumbani, itasafiri hadi Bechar, Algeria kuikabili JS Saoura.

Kama JS Saoura itavuna pointi dhidi ya AS Vita katika mechi zake mbili mfululizo zinazofuata, maana yake Simba itakuwa na wakati mgumu zaidi kwenye mchezo baina yao kwani timu hiyo ya Algeria itakuwa inawania pointi za kuwaweka kwenye nafasi nzuri pia ya kufuzu robo fainali.

Tangu ianze kushiriki mashindano ya Afrika kwa klabu mwaka 2018, JS Saoura haijapoteza mchezo nyumbani kati ya mechi tano ilizocheza ambapo imeshinda nne, imetoka sare mara moja na imefungwa bao moja tu.

Ikitokea kama Simba itafungwa mechi hizo tatu mfululizo maana yake hata ikishinda mchezo wa mwisho nyumbani dhidi ya AS Vita, itakuwa na pointi sita ambazo hazitakuwa na uwezekano wa kuifanya ifuzu hatua inayofuata.

Simba haina rekodi nzuri ya kupata ushindi ugenini inapokutana na timu kutoka mataifa ya Kaskazini kama Misri, Algeria, Tunisia na Morocco ambapo mara zote imepoteza mechi ndani ya dakika 90.

Akizungumzia ugumu wa ratiba ambayo iliyoko mbele yake, kocha wa Simba, Patrick Aussems alisema wako tayari kukabiliana nayo ingawa wanatakiwa kujipanga zaidi.

“Ni somo kwetu na tunatakiwa kurekebisha makosa katika mechi zinazofuata ili tuweze kufanya vizuri, naamini hilo linawezekana hakuna haja ya kukata tamaa,” alisema kocha huyo raia wa Ubelgiji.

Kiungo wa Simba, James Kotei alisema wamejifunza kupitia makosa waliyofanya katika mechi dhidi ya AS Vita na matumaini yao ni kufanya vyema katika mechi zijazo.