TUHUMA ZA AUSSEMS: Wabrazili wageuka kaa la moto Simba

Friday December 6 2019

 

By Thobias Sebastian, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Tuhuma zilizotolewa na aliyekuwa kocha wa Simba, Patrick Aussems kwamba uongozi wa klabu hiyo ulikuwa unaingilia majukumu yake ikiwamo kusajili wachezaji bila ya idhini yake, zimeonekana kuwa kaa la moto kwa mabingwa watetezi hao, huku kwenye mitandao ya kijamii swali la ‘ni nani aliyewanunua Wabrazili?’ likishika kasi.

Aussems ambaye alifutwa kazi isivyotarajiwa klabuni hapo, alidai katika usajili uliopita mchezaji aliyempendekeza ni Francis Kahata pekee miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa.

Pamoja na Kahata, Simba ilisajili wachezaji kadhaa wakiwamo Wabrazili watatu, Tairone Santos, Wilker da Silva na Gerson Fraga ambao viwango vyao vimezua maswali tangu walipowasili na wamekuwa wakitumia muda mwingi kukaa benchi ama majukwaani kutokana na kukosa uhakika wa namba kikosini.

Mchezaji wa zamani wa TP Mazembe, Deo Kanda pia alimwaga wino Msimbazi, pamoja na wazawa Benno Kakolanya, Ibrahim Ajibu na Miraji Athumani ‘Sheva’.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa aliiambia Mwananchi katika mahojiano maalum jana kuwa si vyema kumzungumzia Aussems hivi sasa kwa vile hawako naye tena, lakini akatetea viwango vya Wabrazil hao.

Senzo alisema aliwasiliana na mmoja wa wachezaji wakubwa Afrika Kusini raia wa Brazili ambaye anacheza katika timu ya Mamelodi Sundowns ambaye alicheza na Tairone na kumueleza kuwa ni miongoni mwa mabeki bora wa kati.

Advertisement

“Alichoniambia Tairone alikuwa anakosa muda wa kutosha wa kucheza ndio maana anaonekana kushindwa kudumu katika kiwango bora, lakini kama akipata muda wa kutosha ataonyesha kiwango zaidi ya alivyocheza mwanzo,’’ alisema.

“Nilipojaribu kuzungumza na Aussems alionyesha kutowakubali wachezaji hawa jambo lililosababisha kutokuwapo kwa maelewano kati yao, lakini kwetu tunaamini ni miongoni mwa wachezaji wazuri na bora tulionao katika timu,’’ alisema.

USAJILI MPYA

Senzo alisema mchakato walionao kwa sasa ni kumsaka kocha mkuu mpya, huku pia uvumi ukidai kocha Selemani Matola amesaini mkataba wa miaka mitatu kutoka Polisi Tanzania.

Alisema kuhusu usajili mpya wana majina ya wachezaji kadhaa, ambayo kocha mpya ajaye akiwakubali watawasainisha.

Habari za ndani zinadai kuwa Simba inataka kuongeza mshambuliaji mmoja na tayari ina majina mawili, akiwamo straika wa AS Vita, Tuisila Kisinda na straika mwingine Mganda kutoka katika timu ya KCCA.

Senzo alisema Matola “huenda” ameshasaini mkataba huo wa miaka mitatu, lakini kinachotakiwa ni muda muafaka ili jambo hilo litangazwe akisisitiza Simba wamepanga kuwa na benchi la ufundi imara.

‘’Jambo kama hili la heri wala halina wasiwasi, linaweza kukamilika muda wowote kwani tumefikia katika hatua nzuri ya kulikamilisha,’’ alisema Senzo.

Advertisement