Wabunge Tanzania kulipa Sh3.5 milioni kuishuhudia Taifa Stars Misri

Muktasari:

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameweka kiasi cha fedha wanachotakiwa kulipa wabunge ili kwenda nchini Misri kuishangilia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ inayoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

Dodoma. Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amewataka wabunge kuendelea kujiandikisha ili kwenda kuishangilia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zinazofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumatatu Juni 10, 2019, Ndugai amesema wabunge wanaotaka kukaa siku nne  Misri wanatakiwa kulipia Dola 720 za Marekani (sawa na Sh1.7 milioni).

Amesema wawakilishi hao wa wananchi wanaotaka kukaa siku 10 nchini humo watapaswa kulipia Dola 1,490 (sawa na Sh3.5 milioni).

Msafara wa wachezaji 32 wa Taifa Stars uliondoka nchini Juni 7, 2019  kwenda Cairo Misri kuweka kambi ya maandalizi ya mwisho ya fainali hizo.

Ndugai ametoa maelekezo hayo, akiwataka wabunge kuwafuata wenzao wanaoandikisha majina ya wanaotaka kwenda Misri, akiwemo mwenyekiti wa Bunge Sports Club, William Ngeleja ili kulipia kiasi hicho cha fedha.

Katika fainali hizo Taifa Stars imepangwa kundi moja na Algeria, Senegal na Kenya.