Wachezaji Bayern wakesha baa kabla ya kuitandika Chelsea

London, England. Kipigo cha mabao 3-0 ambacho Bayern Munich ilikitoa kwa Chelsea Jumanne iliyopita kimemuacha hoi nyota wa muziki wa rock, Mmarekani Jon Bon Jovi kutokana na jinsi wachezaji wa klabu hiyo bingwa Ujerumani walivyojiandaa kwa mchezo huo.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 57 yuko London kurekodi wimbo maalumu wa Prince Harry kwa ajili ya Taasisi ya Maveterani wa Jeshi.
Akizungumza na kituo cha redio cha Talk Sport jana Jumatano, mwanamuziki huyo alisema alikuwa katika baa hoteli aliyofikia kama ilivyokuwa kwa wachezaji wa Bayern.
"Nilikuwa na mambo yangu katika baa," Bon Jovi alisema. "Na timu hiyo ilikuwa hapo usiku wa kuamkia jana (Jumatatu) na kwa jinsi-- kwa kutumia nguvu ya whiski na bia-- walivyoizidi nguvu Chelsea, inatoa picha pia kuhusu tabia ya unywaji kwa Chelsea."
Jovi, ambaye alitamba kwa kiwango cha juu mwaka 1987 alipotoa wimbo wake wa "Livin On A Prayer (Kuishi kwa Maombi)", alitania kwamba ushushushu wake wake huenda ukawaweka baadhi ya wachezaji kwenye kitimoto.
"Jamaa wa Bayern bila shaka walikuwa wakichapa whisky na walikuwa ‘wakila bata’ na baadaye walienda kuipiga Chelsea," alisema Jovi. "Nitamuingiza kila mtu kwenye matatizo."
Katika mchezo huo, Bayern ilijipatia mabao yake katika kipindi cha pili kupitia kwa Serge Gnabry aliyefunga mawili na la tatu likiwekwa wavuni na Robert Lewandowski.
Timu hizo zitarudiana Machi 18 kwenye Uwanja wa Allianz Arena