Wachezaji Juventus wakatwa mishahara hisa za klabu zapanda

Muktasari:

Vigogo hao wa soka nchini Italia walitangaza kufanya makato katika mishahara ya wachezaji Jumamosi iliyopita na matokeo yake hisa za klabu zimepanda.

Hisa za Juventus leo zimepanda thamani baada ya uamuzi wa klabu hiyo kukata mishahara wachezaji katika kukabiliana na athari za mlipuko wa virusi vya corona.
Mabingwa hao wa soka wa Serie A walitangaza Jumamosi iliyopita kuwa wamekata mishahara ya wachezaji wao kuanzia Machi hadi Juni baada ya michezo yote nchini Italia kusimamishwa.
Hisa za klabu hiyo zilipanda kwa asilimia 7.94 leo asubuhi katika Soko la Hisa la Milan ambalo limeathiriwa sana na virusi vya corona.
Wachezaji wa Juventus wenye mishahara mikubwa ni pamoja na Christian Ronaldo, ambaye ameshatwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia mara tano na kiungo wa Wales, Aaron Ramsey, ambaye alijiunga na klabu hiyo akitokea Arsenal katika uhamisho ambao haukuwa na ada.
Taarifa ya klabu inasema ilikubaliwa kuwa athari za kiuchumi na kifedha kwa mwaka 2019/20 zinafikia dola 100.5 milioni.
Juventus, ambayo ilikuwa juu ya Lazio kileleni mwa msimamo wa ligi kwa tofauti ya pointi moja kabla ya msimu kusimamishwa Machi 9, iliongeza kuwa kama msimu utamaliziwa mwaka huu, wachezaji wanaweza kulipwa ziada katika miezi hiyo.
Zaidi ya watu 10,000 wamefariki kwa ugonjwa huo wa Covid-19 nchini Italia, idadi ambayo ni kubwa kuliko nchi nyingine yoyote.
Wachezaji katika klabu nyingine kubwa barani Ulaya wamekubali makato katika mishahara yao, zikiwemo klabu za Bayern Munich na Borussia Dortmund zinazoshiriki Bundesliga nchini Ujerumani.