Wachezaji Southmpton waachia mishahara kupambana na corona

Muktasari:

Wachezaji hao hawatapokea mishahara ya miezi mitatu wakati huu nchi ikipambana vikali kudhibiti ugonjwa wa virusi vya corona.

London, Uingereza. Southampton imekuwa klabu ya kwanza ya Ligi Kuu ya England kusogeza mbele malipo ya mishahara ya wachezaji huku kiongozi wa juu wa chama cha wanasoka akisema wanachangia sehemu yao kwa taifa wakati huu wa ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, ulioikumba dunia.
Wachezaji wa Southampton, kocha Ralph Hasenhuttl, wafanyakazi wa benchi la ufundi na wakurugenzi wataachia mishahara yao ya mwezi Aprili, Mei na Juni.
Klabu hiyo ilisema hatua hiyo itasaidia "kulinda hali ya baadaye ya klabu, wafanyakazi wake na jamii wanaoitumikia".
Southampton pia ilisema haitatumia mpango wa serikali kulipa mishahara kwa wafanyakazi wengine.
Uamuzi huo umekuja wakati kuna mzozo kuhusu kama wachezaji wa Ligi Kuu -- ambao wastani wao wa mishahara ni dola 3.7 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh8 bilioni za Kitanzania) -- walazimishwe kuruhusu kukatwa sehemu ya mishahara yao ili kulisaidia taifa.
Bobby Barnes, naibu mtendaji mkuu wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa (PFA), alisema wachezaji wanavishwa ubaya na watu ambao wanapuuzia ukweli kwamba wanasaidia "familia kubwa" nyumbani na nje ya nchi.
Utetezi wa Barnes kwa wachezajui ulikuja baada ya nyota kadhaa, akiwemo nahodha wa Liverpool,Jordan Henderson na wa England, Harry Kane kuanzisha kampeni yao binafsi ya kutafuta fedha Wakala wa Taifa wa Huduma ya Afya (NHS), wakiita #PlayersTogether.
Itahusisha wachezaji wanaotoa michango kwa hiari na mpango huo umesifiwa na NHS kuwa ni wa aina yake.