Wachezaji Yanga kulipwa mishahara yao leo, Lamine abanwa, Sadney aagwa

Tuesday December 10 2019

 

By THOMAS NG'ITU

Dar es Salaam.Mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema wachezaji wake watapokea mishahara yao leo jioni akisisitiza beki Lamine Moro bado ni mchezaji wao.

Dk Msolla alisema tangu wameingie madarakani wamelipa wachezaji wote mishahara na wanadaiwa mishahara ya miezi miwili tu.

"Mpaka leo jioni mishahara itakuwa imeshaingia kwenye akaunti zao, tunakiri kweli hatukulipa, lakini wanalipwa fedha zao," alisema Dk Msolla.

Akizungumzia suala la barua ya beki Mghana Moro mwenyekiti huyo alisema siyo kweli kwamba anatudai miezi mitatu kama anavyodai ila anadai mishahara ya miezi miwili.

"Kweli anatudai lakini sio miezi mitatu, tulimtafuta alipooandika barua, lakini alisema anakuja na kesho yake akaondoka kwenda kwao, lakini bado tunawasiliana naye kumuelezea hali halisi," alisema.

Msolla alisema mchezaji huyo popote atakapokwenda bado ni mchezaji wetu kutokana na bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu.

Advertisement

"Wachezaji wote wa kigeni wana mikataba ya miaka miwili hivyo bado wapo na sisi, mishahara ya miezi miwili kama nilivyosema awali ni kwamba tunawalipa leo jioni tu," alisema

Pia, alisema wamekubali kuachana na mshambuliaji Sadney Urikhob baada ya makubaliano ya pande mbili lakini, David Molinga bado yupo.

"Sadney aliomba kuondoka na tulielewana vizuri na hatudaiani yani tumeachana vizuri, kwa upande wa Molinga ameomba kwenda kwao Ufaransa kwa wiki moja anauguliwa na mwanae ameahidi atarejea na tumemruhusu," alisema.

Dk Msolla alipiga kijembe cha kimtindo kwamba wameendelea kumng'ang'ania Moro kutokana na uwezo wake uwanjani ni tofauti na Sadney.

"Mpira ni mchezo wa wazi sasa utashangaa vipi sisi kumuachia Sadney na kuendelea na Moro," alisema Dk Msolla.

Advertisement