Wadau wachambua kilio cha Zahera Mbeya

Wednesday December 5 2018

 

By Olipa Assa, Mwananchi

Dar es Salaam. Wachambuzi wa soka nchini wametoa tafsiri ya kilio cha Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera aliyelia muda mfupi baada ya kumalizika mchezo kati yao na Prisons ya Mbeya.

Akizungumza jana, nahodha wa zamani wa Yanga ambaye pia ni mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema tafsiri ya kilio cha kocha kina maana kubwa katika mchezo wa soka.

Mayay alisema kitendo cha Zahera kulia hadharani kinaonyesha namna soka lilivyokuwa moyoni mwake na jinsi anavyoguswa na matatizo ya wachezaji wa Yanga.

Alisema mazingira ya maisha magumu wanayopitia wachezaji wa Yanga na matokeo mazuri wanayopata katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara yanaweza kumfikirisha mtu yeyote mwenye hekima na busara.

“Pongezi lazima apewe Zahera, wachezaji na viongozi wachache waliopo, kwa staili hii Yanga itafika mbali na inaweza kutwaa ubingwa ikiwa na ukata, fikiria Prisons ni timu ngumu lakini ameweza kupata pointi tatu Sokoine ni maajabu,”alisema Mayay.

Naye Kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema kwa hali halisi ya kiuchumi wanayopitia Yanga, Zahera anahimili mambo mengi yanayompa uchungu.

“Soka lina hisia kali sana ndio mchezo unaoongozwa kupendwa duniani, mfano mzuri ni mashabiki wanavyokuwa wanazimia uwanjani, kulia kwa Zahera kunaonyesha anavyoipenda kazi yake na vikwazo anavyopambana navyo,” alisema nyota huyo wa zamani wa Taifa Stars.

Akizungumza kwa simu jana, Zahera alisema haikuwa hali yake ya kawaida kulia hadharani na hali hiyo ilitokea kutokana na hisia kali kwa wachezaji wake.

Zahera alisema wachezaji wake wanapitia kipindi kigumu, lakini wameonyesha nidhamu kwa kufuata vyema mafunzo ya benchi la ufundi.

“Ninapokuwa na wachezaji nasimama kwa nafasi ya baba ambaye ana watoto wanaoonyesha juhudi ya kufanya kitu, lakini siwezi kuwatimizia mahitaji yao kwa wakati, siyo kwamba napenda lakini sina cha kuwapa, inafikia hatua kama binadamu naumia sana,” alisema Zahera.

Kocha huyo raia wa DR Congo, alitoa machozi muda mfupi baada ya kumalizika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Prisons ya Mbeya juzi.

Advertisement