Wadau wazungumzia nafasi ya Stars

Sunday April 14 2019

 

By Oliver Albert,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya timu ya Taifa ya Tanzania’Taifa Stars’ kupangwa kundi linalotajwa kuwa la kifo, baadhi ya wadau wa soka wamewatuliza wachezaji wa timu hiyo kwa kuwaambia hawapaswi kuwa na hofu kwani wanaweza wakaishangaza Afrika.

Taifa Stars imepangwa Kundi C pamoja na Senegal, Algeria na Kenya katika Fainali hizo zitakazofanyika kuanzia 21 Juni hadi 19 Julai mwaka huu nchini Misri.

Kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua amekiri kuwa kundi hilo ni gumu hasa dhidi ya Senegal na Algeria lakini amewaambia wachezaji wa Taifa Stars wasihofie majina makubwa ya wachezaji wa timu hizo kwani zinafungika.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema Tanzania inaweza kushangaza katika fainali hizo licha ya wengi kuona kama imepangwa kundi gumu.

“Lazima watu wajue hakuna timu ndogo kwenye fainali hizo mashindano kwani mwaka 2015 watu wote walikuwa wakisema Algeria, Senegal zitabeba kombe lakini uwanjani mambo yakawa mengine.

Kocha wa Prisons, Mohammed Adolph Rishard alisema licha ya kwamba Tanzania imepangwa katika kundi gumu lakini inaweza kufanya vizuri na kufika hata fainali.

“Kundi gumu kwetu lakini ni kundi lenye mvuto kwani lina mchanganyiko wa ladha ya soka kutoka Afrika Mashariki, Afrika Magharibi na Kaskazini.

Advertisement