Wakati Chadema wakikomaa, Karia, mwenyewe wala...

Muktasari:

Chadema imeandika barua kwenda Fifa, ikimshtaki Karia kwa kutoa kauli za kibaguzi na unyanyasaji.

Dar es Salaam. Baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kupeleka barua Fifa ikilalamikia kauli za kibaguzi za Rais wa TFF, Wallace Karia, rais huyo amesema hajui lolote na wala hataki kuongelea hizo habari.

Chadema imeandika barua kwenda Fifa, ikimshtaki Karia kwa kutoa kauli za kibaguzi na unyanyasaji.

Barua hiyo ya kurasa mbili, iliyosainiwa na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imeonyesha masikitiko yake kwa kitendo cha Karia kutumia wa soka kuonyesha chuki na ubaguzi dhidi ya Tundu Lissu ambaye Septemba 7, 2017 alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30.

“Tunaandika barua kuelezea masikitiko yetu na kupinga kauli iliyotolewa na Rais wa TFF, Wallace Karia inayounga mkono uvunjaji haki za binadamu, uhuru wa kuzungumza na kuchochea ubaguzi wa kisiasa jambo ambalo ni kinyume na miiko ya mchezo wa mpira wa miguu unaosimamiwa na Fifa,” imeeleza barua hiyo.

Barua hiyo ambayo pia nakala yake imepelekwa Shirikisho la Soka Afrika (Caf) na Karia mwenyewe, imeambatanishwa pia na ushahidi wa kipande cha video kinachomuonyesha Karia akitoa kauli hiyo.

Jumamosi, Februari 2, mwaka huu akiwa Arusha katika mkutano mkuu wa TFF, Karia alikemea watu wenye tabia alizoziita za ‘u Tundu Lissu’ katika soka, kuwa kamwe hatokubali kuona wakiendelea kukosoa uongozi wa TFF.

Hata hivyo baada ya mkutano huo, alipotakiwa kutoa ufafanuzi, Karia alisema alimfananisha Lissu na aliyekuwa Makamu wa Rais wa TFF, Michael Wambura kutokana na mambo wanayoyafanya kwenye vyombo vya habari na majukwaa mbalimbali

“Nikamlinganisha Wambura na Lissu, lakini kama hii kauli imewakera wengine naomba samahani ila nimewalinganisha kutokana na kuhama hama kwenye vyombo vya habari kutoa kauli za kuwadhalilisha viongozi waliochaguliwa kihalali,” alisema Karia.

Alipoulizwa kuhusu Chadema kumshitaki Fifa Karia alijibu kwa kifupi: “Sijui habari zozote na wala siwezi kuongelea, nilishatoa ufafanuzi siku ile inatosha, siendelei tena.”

Licha ya kutoa ufafanuzi huo Chadema walitoa taarifa kumtaka Karia kuomba radhi kwa kuwa,alitumia jina la Lissu kwa lengo la kumchafua.

Taarifa hiyo ilisema kuwa Chadema haina mpango wa kuingia kwenye ugomvi na TFF wala wadau wa michezo hivyo, ni vyema akatekeleza agizo hilo la kumuomba radhi Lissu kabla ya hawajachukua hatua za kisheria.

Wasikie Chadema/Karia.

Gazeti hili liliwauliza Chadema kwa nini hawakupekela kwanza malalamiko yao kwenye kamati za TFF kama kanuni na sheria zinavyotaka na badala yake wakaenda moja kwa moja Fifa ilihali Kamati za Nidhamu na Maadili za TFF ni kamati huru na haziingiliwi na yeyote?.

Mkurugenzi wa Itifaki,Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema,John Mrema alijibu kwa kusema Hawakuona sababu ya kuanzia kupeleka malalamiko yao kwa Shirikisho la Soka la ndani kwa sababu aliyesema ni rais wa TFF.

“Rais wa TFF alikuwa anahutubia kikao cha TFF ambako hao wajumbe wa Kamati ya rufaa, wajumbe wa Kamati za maadili walikuwa sehemu ya kikao kilichokuwa kinahutubiwa.

“Kwa hiyo wao tunaamini wataenda kuwa mashahidi kule Fifa kwa sababu walimsikia raisi wa TFF akisema, badala ya kuwatwika wao mizigo ili washughulike na Rais ambaye atawazidi nguvu basi wao watakwenda kuwa mashahidi Fifa.

“Hatujakata Rufaa Fifa tumemshtaki moja kwa moja.Ni wajibu wa Fifa waamue kuchukua hatua au kutochukua.Tumeshawapelekea barua na wameipokea jana(juzi) kwa hiyo tunasubiri uamuzi wao utakuwa nini.

“Wakitumbia kwamba tulitakiwa tuanzie ndani,sisi sio chama cha mpira, yaani tungekuwa Shirikisho la Mpira au Chama cha soka cha Mkoa ndio tungefuata hizo hatua tushtaki ngazi kwa ngazi na tukishindwa ndio twende Fifa lakini sisi ni Chama cha Siasa kwa hiyo tumeamua kwenda moja kwa moja ambako mamlaka yake ya nidhamu ipo”alisema Mrema

Naye Karia alisema hajasikia habari za Chadema kutinga Fifa wala hataki kuziongelea.

“Sijui habari zozote na wala siwezi kuongelea .Nilishatoa ufafanuzi siku ile inatosha,siendelei tena”alisema Karia kwa ufupi.