Wanamichezo wamlilia Mo Dewji

Friday October 12 2018

 

By Oliver Albert, Edo Kumwembe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam/Cape Verde. Muda mfupi baada ya mfanyabiashara maarufu nchini Mohammed Dewji ‘Mo’ kutekwa, wadau wa michezo wamepokea kwa masikitiko taarifa hizo.

Dewji ambaye ni mwekezaji wa Klabu ya Simba, alitekwa na watu wasiojulikana jana asubuhi muda mfupi, baada ya kuteremka ndani ya gari yake akielekea Hoteli ya Colosseum, Dar es Salaam kufanya mazoezi ya viungo ‘gym’.

Tukio hilo limewapa simanzi wadau mbalimbali wa michezo ambao walitoa kauli tofauti ikiwemo ya kuwataka Polisi kutumia taaluma yao kuhakikisha mfanyabiashara huyo anapatikana akiwa salama.

Akizungumza akitokea Cape Verde jana, Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, ametoa rai kwa mashabiki wa klabu hiyo na wanamichezo kumuombea dua Dewji apatikane.

Try Again ni miongoni mwa wadau waliokwenda Cape Verde kuiunga mkono Taifa Stars inayocheza leo usiku mchezo wa kufuzu fainali za Afrika.

“Jambo linalotakiwa kufanywa ni kumuombea dua ili mwenzetu awe salama huko alipo, Polisi wanafuatilia kwa ukaribu suala hilo,”alisema Try Again.

Alisema Dewji alimpigia simu juzi kuomba mchango wa mawazo kuhusu masuala mbalimbali baada ya mfanyabiashara huyo kumaliza kikao cha Bodi.

Pia baadhi ya wachezaji wa Simba John Bocco, Shomari Kapombe, Aishi Manula na Shiza Kichuya walionyesha kuguswa na tukio la kutekwa Dewji.

Mratibu wa Yanga, Hafidh Saleh alisema wamepokea kwa masikitiko taarifa ya kutekwa Dewji kwa kuwa halikuwa tukio la kawaida.

“Sisi na Simba siyo maadui ni watani kwa hiyo jambo lililomtokea MO limetuumiza na tunamuombea kwa Mungu apatikane akiwa salama aendelee na majukumu yake mengine,” alisema Hafidh.

Kocha wa zamani wa Cargo, Bandari na Yanga, Kenny Mwaisabula alisema ameshtushwa na taarifa za kutekwa Mo na ameviomba vyombo vya dola kuongeza nguvu ya kumtafuta ili apatikane akiwa salama.

“Nimeshitushwa na tukio hili, nimejiuliza kwa nini Mo, tajiri wa kwanza kijana Afrika atembee bila walinzi katika nchi ambayo matukio ya utekaji yanazidi kushamiri wakati mwanamuziki Diamond Platnumz ana walinzi wanamzunguka kila anapokwenda.

“Natumaini vyombo vya dola vinahangaika kusaidia upatikanaji wake na tunamuombea apatikane akiwa salama,”alisema Mwaisabula.

Kocha Mohammed ‘Adolph’ Rishard alisema Dewji ni mwanamichezo aliyejipambanua katika sekta ya michezo na kutekwa kwake ni tukio baya.

Beki wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Boniface Pawasa amemtakia kheri Dewji arejee salama kuendelea na majukumu yake ya kiutendaji.

“Nikiwa mchezaji wa zamani wa Simba na mwanachama naomba huko aliko awe salama, hatujui amekweda wapi na anafanya nini muhimu ni kumuombea arudi akiwa mzima,”alisema Pawasa.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), Phares Magesa alisema wanalaani kwa nguvu tukio hilo lililomtokea mwanamichezo mwenzao na wanamuombea apatikane akiwa salama.

“Tukio hilo limetusikitisha wote na tunalaani vikali. Tunaomba vyombo vya dola vishughulikie na kuhakikisha anapatikana katika hali ya usalama,”alisema Magesa.

Mchezaji wa zamani wa Yanga,Sekilojo Chambua alisema matukio ya utekaji yanayozidi kushamiri nchini hayaleti taswira nzuri kwa nchi.

“Haya matukio naona yanazidi kushamiri na hayaleti taswira nzuri kwa nchi na hao waliofanya tukio hilo wasakwe Mo ni mtu anayefahamika kama mfanyabiashara, mwanamichezo na hata mbunge wa zamani,” alisema Chambua.

Kocha Mrage Kabange alisema anamuombea mfanyabiashara huyo apatikane akiwa salama na ametoa wito kwa vyombo vya usalama kuongeza kasi ya kumtafuta.

Uwekezaji Simba

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, chini ya ushawishi wa Dewji, Kampuni zake za METL ziliingia mkataba wa kuidhamini Simba ambao ulichangia klabu hiyo kupata mafanikio katika mashindano mbalimbali ndani na nje.

Simba ikiwa chini ya Dewji ilitwaa Kombe la Afrika Mashariki na Kati mwaka 2002, ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara mara tatu, Kombe la Tusker mara tatu na kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2003.

Baada ya kukaa muda mrefu bila kujishughulisha na soka, Julai 2016, Dewji alitangaza nia ya kutaka kuwekeza katika klabu ya Simba kwa kiwango cha hisa asilimia 50 alizotangaza atanunua kwa Sh20 bilioni.

“Shabaha yangu ni kuitoa klabu kwenye bajeti ya bilioni 1.2 hadi bilioni 5.5. Mashabiki wa Simba wanahitaji mafanikio ya haraka. Lazima tusajili vizuri na tuajiri makocha wazuri. Ukitenga bilioni nne kwa mwaka, tayari umewazidi wapinzani wako Azam na Yanga,” alinukuliwa Dewji.

Dhamira ya Dewji ilichangia kubadilishwa katiba na kupatikana mpya ambayo inabariki mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji na kuifanya Simba kuwa kampuni ambapo mfanyabiashara huyo alishinda zabuni ya kuwa mwekezaji kwa asilimia 49 ya hisa.

Advertisement