Wanasheria wafunguka uchaguzi Yanga

Wednesday January 16 2019

 

By Imani Makongoro, Thomas Ng’itu, [email protected]

Dar es Salaam. Muda mfupi baada ya Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kutangaza kufanyika uchaguzi mdogo wa Yanga ndani ya siku saba kuanzia jana Jumanne, wanasheria wameipa neno TFF.

Jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Ally Mchungahela alisema mchakato wa uchaguzi wa klabu hiyo utaendelea ndani ya siku saba kwa kuwa baadhi ya waliofungua kesi kupinga siyo wanachama halali wa Yanga.

Wakati Mchungahela akitoa kauli hiyo, baadhi ya wanasheria wamesema TFF iko sahihi kuendelea na mchakato huo, lakini wahakikishe wanazuia oda iliyopo mahakamani ndipo mchakato huo uendelee.

Aliyewahi kuwa mwanasheria wa Yanga, Frank Chacha alisema TFF iko sahihi, lakini kabla ya kuendelea na mchakato huo, inapaswa kutengua oda ya mahakama.

“Kama wataendelea na uchaguzi wakati oda iko mahakamani, mwenyekiti na baadhi ya watu wengine wa kamati wanaweza kushitakiwa kwa kuidharau mahakama, hivyo kilichopo ni TFF kwenda kuomba wasikilizwe kabla ya tarehe iliyopangwa na mahakama (Januari 24, 2019),” alisema Chacha.

Mchungahela alipotakiwa kutoa ufafanuzi wa kisheria kuhusu kuondoa oda ya mahakama, alisema kuwa mambo yote yatafanyika ndani ya siku saba kabla ya mchakato wa uchaguzi kuendelea.

“Taratibu zote za kisheria zitafuatwa, lakini uchaguzi wa Yanga uko palepale, ndani ya siku saba tulizosema kila kitu kuhusu uchaguzi na tarehe rasmi vitajulikana na kampeni kwa wagombea zitafanyika kwa siku moja,” alisema Mchungahela.

Akizungumzia namna uchaguzi huo ulivyoahirishwa, Chacha ambaye ni wakili alisema hakuona sababu ya mwanachama kupinga kadi mpya za Benki ya CRDB au Benki ya Posta wakati Klabu ya Yanga ndiyo iliingia mkataba na benki hizo.

“Hakukuwa na sababu ya mwanachama kupinga kadi zile wakati klabu ndiyo iliingia mkataba, hamasa ilikuwa kubwa, sijui hapo mwanachama anapingaje mkataba wa klabu, halafu isitoshe Yanga inakwenda wapi? mbele au inarudi nyuma kwa hicho wanachopinga” alihoji Chacha.

Mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye aliomba hifadhi ya jina alisema idadi ya wanachama wa kadi za kitabu ni 2,000 na kadi za benki ni 15,000 na wote wanatambulika kwa kuwa wametumia kadi hizo katika uchaguzi zaidi ya mbili wa klabu hiyo.

Mwanasheria nguli na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dk Damas Ndumbaro alisema kama suala hilo liko mahakamani lazima mhimili huo uheshimiwe ingawa mchakato wa uchaguzi utategemea amri ya mahakama ikoje.

“Pia, kuna uwezekano pande mbili zilizokuwa zinakinzana zimefikia makubaliano nje ya mahakama kwa maana hiyo hapo tena hakuna kitakachokwamisha uchaguzi huo,” alisema Dk Ndumaro.

Mwanasheria mwingine, Nestory Mwandiba alisema TFF iko sahihi kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Yanga.

“Klabu haina mwenyekiti, haina makamu mwenyekiti na wajumbe wanne, hiyo kamati ya uchaguzi ya Yanga ingeteuliwa na nani, TFF iko sahihi kwenye hilo, lakini kilichopo ni kuhakikisha inafuata taratibu za kisheria kabla ya kwenda kwenye uchaguzi,” alisema Mwandiba.

Licha ya Mchungahela kusisitiza baadhi ya waliofungua kesi siyo wanachama halali, Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Samwel Lukumay alisema hawezi kuzungumzia uhalali wa wanachama hao hivi sasa kwa kuwa ni masuala ya kisheria.

Manji

Jana Jumanne ndiyo siku ambayo Baraza la Wadhamini wa Yanga lilitangaza, Yusuf Manji angeanza kazi rasmi kuendelea na majukumu yake ndani ya klabu kongwe nchini.

Hata hivyo kufikia saa 8:00 mchana, hali ilikuwa ya utulivu Makao Makuu ya Yanga yaliyoko makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam huku maofisa wachache wakiendelea na shughuli zao akiwemo Kaimu Katibu Mkuu, Omari Kaya.

Awali, Uchaguzi wa Yanga uligubikwa na utata baada ya Yanga, Serikali na TFF kuvutana kuhusu nafasi ya mwenyekiti.

Advertisement