Waogeleaji waula mashindano ya dunia

Dar es Salaam. Shirikisho la Kuogelea la Kimataifa (FINA), limetangaza neema kwa waogeleaji wa Tanzania kufuzu kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika baadaye mwaka huu Gwangju, Korea.

Shirikisho hilo limetoa baraka kwa Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) kutumia mashindano ya Taifa kutoa viwango vya kufuzu kushiriki mashindano ya dunia.

Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa TSA kupewa fursa ya kutumia mashindano ya Taifa kupata viwango vya kufuzu mashindano ya dunia.

Katibu Mkuu wa TSA, Inviolata Itatiro alisema wamepokea barua ya FINA iliyowaruhusu kutumia mashindano ya Taifa kupata viwango vya mashindano ya dunia.

Katika barua hiyo, FINA imeitaka TSA kuhakikisha waogeleaji watakaochuana kwenye mashindano ya Taifa wanafikia muda ambao FINA imeuweka wa kufuzu kushiriki mbio za dunia.

“Waogeleaji wanapaswa kufikia muda A au B (muda bora zaidi au ule wa kawaida wa kufuzu) na mara mtakapomaliza mashindano ya Taifa, rekodi hizo zitumwe haraka FINA,” ilieleza barua hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa FINA,Cornel Marculescu.

Kwa mujibu wa Inviolata mashindano ya Taifa yatafanyika Aprili katika mkoa ambao utatangazwa baadaye.

Akizungumzia nafasi hiyo, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) Filbert Bayi, alisema haijawahi kutokea nchini, hivyo itakuwa fursa kwa TSA.

“Mashindano ya kufuzu ni vyama vyenyewe na mashirikisho yao ya kimataifa, hivyo kama wamepewa itakuwa fursa nzuri kwao.

“Ingawa pia itategemea na uwanja au bwawa litakalotumika, hiyo itakuwa fursa nzuri kwao kufuzu kushiriki mashindano ya dunia na kule kwenye mashindano ya dunia, kupambana ili kufuzu Olimpiki 2020,” alisema Bayi.