Wasafi waja na 'Ndondo yao' bingwa kulamba Sh 20milioni

Muktasari:

Chama cha Soka mkoa wa Temeke (Tefa) kwa kushirikina na Wasafi media kimeandaa mashindano ya Kivumbi Cup mshindi ataondoka na Sh20 milioni.

Dar es Salaam. Chama cha Soka mkoa wa Temeke (Tefa) kwa kushirikina na Wasafi media kimeandaa mashindano ya mpira wa miguu ya 'Kivumbi Cup' chini ya miaka 18 na bingwa wake ataondoka na Sh20 milioni.

Akizungumza leo Alhamisi Februari 27,2020 mratibu wa mashindano hayo Said Fella ‘Mkubwa Fella’, amesema lengo la kufanya mashindano hayo ni katika kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana katika soka.

Mkubwa Fella amesema wakati mshindi wa kwanza akiondoka na Sh20 milioni wa pili ataondoka na Sh10 milioni na watatu Sh5milioni.

Wakati droo ya nani atacheza na nani itafanyika Machi 2, 2020 huku mashindano yenyewe ambayo kauli mbiu yake ni 'Thamini kipaji, mpira ni ajira' yakitarajiwa kuanza rasmi Machi 7.

"Mashindano haya yatafanyika kwenye Uwanja wa Bandari na kushirikisha timu 32.

"Timu zitakazohitaji kushiriki zitapaswa kwenda kuchukua fomu katika ofisi za Tefa kwa gharama ya Sh50,000.

Washindi wengine watakaopewa zawadi ni kipa bora, mwamuzi bora na mchezaji bora kila moja ataondoka na Sh500,000.

Katibu kamati ya mashindano (Tefa), Mbaraka Mohamed amesema wameyapokea mashindano hayo malengo yake  ya kuendeleza na kukuza vipaji yameshawishi.

Mohamed amesema pamoja na mashindano hayo kuandaliwa na Tefa, lakini timu kutoka maeneo yote ya Dar es Salaam azitaruhusiwa kushiriki.

Mjumbe wa kamati, Maulid Kitenga amesema katika timu zitakazoshiriki, zitaruhusiwa kuweka wachezaji watano wanaocheza klabu kubwa jambo litakalosaidia kuleta hamasa katika mashindano hayo.