VIDEO: Waziri Mkuu Majaliwa awapa siku 4 wanunuzi wa korosho kumuandikia barua

Muktasari:

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku nne kwa wanunuzi wa korosho waandike barua kwake, wakieleza kiasi cha tani za zao hilo wanazohitaji na lini watazichukua.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku nne kwa wanunuzi wote 35 waliojiandikisha kununua korosho, wawe wamepeleka barua katika ofisi yake,  wakionesha kiasi cha tani wanazohitaji na lini watazichukua.

Majaliwa ametoa ametoa tamko hilo la Serikali kupitia Televisheni ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) leo Ijumaa Novemba 9, 2018, kutokea ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema baada ya kupita siku hizo, Serikali italazimika kufuta usajili kwa wote waliojisajili kununua zao hilo, kwa sababu walikubaliana kwenda kununua, lakini hali inayoonekana sasa ni kama kumkomoa mkulima kitu ambacho amesema Serikali haitakubaliana nacho.

“Mwenye nia ahakikishe katika siku hizo nne, iwe ndio mwisho wa kununua korosho na waandike barua kwani ofisi yangu ipo wazi saa 24, wana nafasi ya kuleta barua wakati wowote, wakionesha nia yao na kiwango wanachokihitaji, zaidi ya hapo Serikali haitoruhusu kampuni yoyote kununua korosho tena” amesema Majaliwa.

Kauli hii imekuja wakati wakulima wa korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara, wakiwa bado hawajui hatima ya zao hilo, kutokana na bei kutetereka nchini ambapo minada ya korosho iliyotakiwa kufanyika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, imesitishwa baada ya wanunuzi kutofika mnadani.

Awali, wakulima wa zao hilo wa mikoa hiyo waligoma kuuza wakilalamikia bei ndogo, ikilinganishwa na ile ya msimu uliopita, jambo lililosababisha Serikali kuingilia kati na kuwashawishi wafanyabiashara kununua korosho kwa bei isiyopungua Sh3,000 kwa kilo.