Waziri Mwakyembe awaomba wadau kuisaidia Tembo Worries

Muktasari:

  • Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Dk Harrison Mwakyembe amewataka Watanzania kuungana kuisaidia timu ya wenye ulemavu ili ifanye vizuri katika mashindano mwezi huu yatakayofanyika nchini Tanzania.

Dodoma. Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amewataka Watanzania kusimama kwa pamoja kwa ajili ya kuisaidia timu ya mpira kwa wenye ulemavu Tembo Worries ili ifanye vizuri katika mashindano mwishoni mwa Juni 2019.

Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo  leo Jumanne Juni 4,2019 alipoendesha kikao kwa wabunge wenye ulemavu na kamati waliyoiunda kwa ajili ya kuisaidia timu hiyo.

Tembo Worries mwishoni mwa Juni 2019 itashiriki mashindano ya mpira wa miguu kwa wenye ulemavu yatakayoshirikisha nchi tano za Afrika ambapo Tanzania Bara ikiwa ni mwenyeji.

“Kila Mtanzania mwenye uwezo anatakiwa kuisaidia timu hii, lazima tufanye vizuri kwa sababu nia ya kufanya hivyo tunayo, siyo lazima uwe na kikubwa hata kidogo ulichonacho ni muhimu kwani unatakiwa hata kuiombea timu yetu,” amesema Dk Mwakyembe.

Waziri Mwakyembe amesema mashindano hayo ni heshima na faraja kwa Watanzania kwakuwa kwa mara ya kwanza yanafanyika katika ardhi ya Tanzania hivyo itakuwa jambo la kushangaza kama wenyeji wataingia uwanjani bila kuwa na maandalizi ya kutosha.

Kuhusu wabunge amewataka kuendelea kuunga mkono timu hiyo huku akitumia muda mwingi kupiga simu kwa wadau mbalimbali kwa ajili ya kuomba misaada.

 

 

 

Mwenyekiti wa wabunge wenye ulemavu, Riziki Lulida amesema timu hiyo inataraji kuingia kambini Juni 10, 2019 kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mashindano licha ya kuwa walishaanza mazoezi siku nyingi.

Kwa mujibu wa Lulida, zaidi ya Sh700 milioni zinahitajikia kwa ajili ya gharama nzima za mashindano hayo ingawa walishaanza mazoezi siku nyingi kwa ajili ya kujifua na michezo ikiwemo mpira wa miguu.