Wenger kumbe anaitaka Bayern

Muktasari:

Kocha huyo Mfaransa mara kadhaa aligoma kustaafu kazi hiyo tangu alipoachana na Arsenal Mei 2018 akisema hatakuwa na kazi nyingine ya kufanya zaidi ya kuwa kocha.

PARIS, UFARANSA. ARSENE Wenger bado hajaanza mazungumzo na Bayern Munich kwa ajili ya kwenda kuwa kocha, lakini mwenyewe amethibitisha kwamba amejiweka tayari kwa ajili ya kuchukua kibarua hicho.

Kumekuwa na uvumi unaomhusisha kocha huyo wa zamani wa Arsenal na kibarua cha kwenda kuinoa Bayern Munich hadi mwisho wa msimu.

Wenger aliachana na kibarua cha kuinoa Arsenal na mikoba yake ikachukuliwa na Mhispania, Unai Emery.

Kocha aliyekuwa akipewa nafasi hapo awali, Ralph Rangnick haonekani kuwa tayari kwenda kurithi mikoba ya Niko Kovac, aliyefutwa kazi huko Allianz Arena na sasa, Wenger amekuwa na nafasi kubwa.

Kocha huyo Mfaransa mara kadhaa aligoma kustaafu kazi hiyo tangu alipoachana na Arsenal Mei 2018 akisema hatakuwa na kazi nyingine ya kufanya zaidi ya kuwa kocha.

Alipoulizwa kama anavutiwa na kibarua cha kuinoa Bayern, kocha huyo Mfaransa alijibu: “Bila shaka.”

Wakati akifanya uchambuzi kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya juzi Jumatano, Wenger alikiri tena kwa kusema anakaribisha dili hilo, lakini mazungumzo bado hayajaanza.

“Siwezi kukataa kuzungumza na Bayern Munich kwa sababu nafahamiana na watu wanaoongoza klabu ile kwa miaka 30. Nilikaribia kabisa kwenda Bayern miaka mingi iliyopita,” alisema.

“Kwa wakati huu, mazungumzo bado hayajaanza. Hatujazungumza chochote na sifahamu kama jambo hilo litatokea.”

Bayern inahitaji kocha wa muda mwenye uzoefu ili kuweka mambo vizuri kabla haijamchagua kocha wa kudumu, ambapo Thomas Tuchel au Erik ten Hag mmoja wapo anaweza kupewa nafasi.

Bayern Munich ililazimika kuachana na kocha wake Niko Kovac baada ya kufungwa mabao 5-1 ilipocheza dhidi ya Eintrachat Frankfurt.