Wiki ya jasho na damu kwa Simba

Dar es Salaam. Baada ya Simba kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC jana, silaha zao wanazielekeza kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo watacheza dhidi ya UD Songo ya Msumbiji Jumapili ijayo.

Hata hivyo, kwa wiki nzima Wekundu hao wa Msimbazi walikuwa wakijifua katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa jana na pia dhidi ya UD Songo jijini hapa.

Katika mazoezi ambayo Mwananchi liliyashuhudia wachezaji walikuwa wakitengeneza muunganiko huku wakiimarisha uwajibikaji wa mchezaji mmoja mmoja.

Kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems alikuwa akiwagawa katika makundi tofauti yaliyolenga kuwaweka fiti kuanzia mikononi, ambapo mwanzo wa mazoezi walikuwa wakivuta vifaa fulani kwa ajili ya kuimarisha mikono ilhali miguuni walikuwa wakifanyishwa mazoezi maalumu ya kuruka viunzi.

Pia walitengenezewa ushindani wa wao kwa wao pindi walipokuwa wakifanya zoezi hilo.

Zoezi lingine lilikuwa ni lile la kukabiliana na kocha wa makipa, Mohammed Mwarami aliyekuwa akiwarushia mpira na kuuwania kisha kupiga shuti golini ambako alikuwepo kipa Benno Kakolanya.

Kila baada ya kumalizika kwa mazoezi ambayo waligawanya kwenye makundi kulingana na programu ya siku husika, Aussems akisaidiwa na wenzake waliwagawa tena wachezaji hao na kutoa maelekezo ya kiufundi.

Kocha huyo alionekana kuwasihi wachezaji wake kuacha mipira kwa haraka kila wanapokuwa nayo huku wakitafuta nafasi za kupokea tena.

Katika zoezi hilo, Cletous Chama na Francis Kahata ni miongoni mwa wachezaji walioonekana kumudu vyema aina hiyo ya mazoezi kila yalipokuwa yakifanyika.

Naye Gadiel Michael alikuwa akifanya vizuri kwenye ukabaji pamoja na Pascal Wawa, Haruna Shamte na Shomary Kapombe japo nao waliwajibika kuucheza mpira kwa nafasi pindi upande wao ulipokuwapo.

Kocha Aussems aliutumia mchezo wa jana kama sehemu ya kujiandaa na mchezo wa Jumapili ambao wanatakiwa kushinda ili kuhakikisha wanaingia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa.

Baada ya Simba kurejea kutoka Msumbiji wiki iliyopita ambako walibanwa mbavu na wenyeji wao kwa kutoka suluhu, wachezaji walifikia mazoezini ambapo katika siku za mwanzoni mwa wiki kocha alikuwa akikinoa kikosi chake hasa safu ya ushambuliaji inayoongozwa na mfungaji bora wa msimu uliopita Ligi Kuu Bara, Meddie Kagere.

Kagere na Bocco ambao walicheza pamoja huko Msumbiji kwenye mchezo wa kwanza ndani ya siku nne za mazoezi hayo walikuwa wakichezeshwa pamoja huku kukiwa na maelekezo maalumu kwao ya namna ya kufunga mabao.

Msimu uliopita Simba ilikuwa ikitumia washambuliaji watatu akiwemo Okwi, hivyo kuondoka kwake ni kama kumemfanya Aussems kuwa na namna mbadala ya uchezaji huku akiwategemea Bocco na Kagere.

Katika mchezo wa tamasha la Simba Day, Aussems alimtumia Kagere dhidi ya Power Dynamos ambapo alionekana kufanya vizuri kwa kuwafunga mabao matatu.

Akizungumzia safu yake ya ushambuliaji, Aussems alisema bado iko imara licha ya kuondoka Okwi na inaweza kulithibitisha hilo kwenye mchezo wao wa marudiano dhidi ya UD Songo utakaochezwa Uwanja wa Taifa.

“Namna ya kucheza ugenini ni tofauti na nyumbani, nani ataanza kwenye kikosi cha kwanza itategemea na utimamu wao pale nitakapokuwa nafanya machaguo ya mwisho muda mfupi kabla ya mchezo,” alisema Aussems.

“Wanaweza kuendelea kufunga mabao mengi hata msimu huu kama ilivyokuwa msimu uliopita, siku chache zilizopo mbele yetu tutazitumia kuendelea kuijenga timu.”