Wozniack, Konta wang’oka Pan Pacific Open

Muktasari:

  •  Ni baada ya kushindwa katika raundi ya pili  

Tokyo, Japan. Mastaa wa tenisi kwa wanawake Johanna Konta wa Uingereza na Caroline Wozniack kutoka Denmark wameendelea kuboronga katika mashindano ya mwaka huu.

Konta mchezaji namba moja kwa ubora Uingereza na Wozniack nyota namba moja wa zamani kwa ubora duniani, jana waling’olewa katika raundi ya pili ya mashindano ya wazi ya Pan Pacific Open, yanayoendela nchini Japan.

Donna Vekic kutoka Croatia alimshinda Konta kwa seti mbili ikiwa ni muendelezo wa nyota huyo kufanya vibaya kwa mwaka huu akiwa hajavuka raundi ya 16 bora katika mashindano yoyote, wakati Camila Giorgi wa Italia alimshinda Wozniacki baada ya kumfunga kwa seti mbili pia.

Licha ya Konta kuuanza mwaka akiwa ndani ya kumi bora, ameporomoka hadi nafasi ya 43 na kama hatazinduka anaweza kuumaliza mwaka akiwa nje ya 100 bora. Baada ya kukubali kichapo cha 6-3, 7-5.

Katika mchezo mwingine Camila Giorgi aliwaduwaza wengi kwa umahiri wake aliposhinda mchezo wa sita kati ya minane aliyocheza hivi karibuni akimuangusha Wozniacki na kutinga robo fainali ya Pan Pacific Open kwa ushindi wa 6-2, 2-6 na 6-4.

Nyota mwingine namba moja wa zamani kwa wanawake, Victoria Azarenka wa Belarus alimshinda Ashleigh Barty wa Australia kwa seti mbili za 6-4 6-2 huku Barbora Strycova wa Jamhuri ya Czech akimng’oa Anett Kontaveit wa Estonia kwa 7-6 (7/5) 3-6 7-5.

Mvua kubwa iliyonyesha uwanjani hapo ililazimisha kuahirishwa kwa mchezo uliomhuhusisha bingwa mtetezi wa mashindano hayo, Jelena Ostapenko wa Latvia dhidi ya Ekaterina Alexandrova wa Russia na sasa utachezwa leo.

Huko China yanakoendelea mashindano ya Guangzhou Open, Andrea Petkovic wa Ujerumani alitinga nusu fainali yake ya pili kwa mwaka huu alipomshinda Vera Lapko kwa 6-1, 6-2 huku, Bernarda Pera naye akitinga nusu fainali kwa kumshinda Aleksandra Krunic.