Yaliyompata Aussems ndani ya Simba SC kumkuta Sven

Muktasari:

  • Tangu ametua nchini mwishoni mwa mwaka jana na kupewa kazi ya kukinoa kikosi hicho akichukua nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alionekana kuwagawa mashabiki na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo

MASHABIKI wa Simba ni kama wameanza kuonyesha wasiwasi na ubora wa kikosi chao kwa sasa. Huko kwenye mitandao povu limekuwa kubwa sana. Lakini, mambo ambayo hawafahamu ni kuwa huko ndani ya benchi la ufundi hakuko shwari hata kidogo.

Habari ambazo Mwanaspoti limezinasa na kuthibitishwa na baadhi ya vigogo ndani ya klabu hiyo ambao hawakupenda kutajwa majina gazetini ni kwamba, benchi la ufundi halizungumzi lugha moja kutokana na kuwepo kwa mpasuko mkubwa.

Tangu ametua nchini mwishoni mwa mwaka jana na kupewa kazi ya kukinoa kikosi hicho akichukua nafasi ya Mbelgiji Patrick Aussems, Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck alionekana kuwagawa mashabiki na baadhi ya viongozi wa klabu hiyo.

Wapo viongozi na mashabiki ambao walionyesha wasiwasi na wasifu wake, lakini kwa kuwa ni mapendekezo ya baadhi ya Wajumbe wa Bodi ya Simba, mambo yakaachwa yaende kama yalivyo.

Lakini, baada ya kuanza rasmi kibarua chake Desemba 12, mwaka jana, taratibu tabia za Sven zikaanza kujionyesha ndani ya kikosi hicho.

Licha ya kuanza kampeni za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao Aussems aliwapa Simba msimu uliopita, Sven alianza kwa ushindi dhidi ya AFC Arusha, Lipuli kisha Ndanda kabla ya kutoka sare na Yanga ya mabao 2-2.

Habari kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa, Sven amekuwa mkali wakati anapotoka maelezo mazoezini na wakati mwingine ikidaiwa kuwa lugha anayotumia imekuwa ikiwaudhi makocha wenzake na baadhi ya wachezaji.

Imeelezwa kuwa wakati Simba ikijiandaa na mchezo na Yanga, Sven alitibuana na kiungo wake Sharaf Eldin Shiboub.

Shiboub aliingia kwenye ugomvi na Sven, baada ya kupewa maelekezo huku akiwa ameshikwa shingoni jambo ambalo hakulifurahia. Pia, imeelezwa kuwa matumizi mabaya ya lugha yamevuka mipaka hadi kwa wasaidizi wake katika benchi la ufundi. Mbali na Sven, makocha wengine wanaounda benchi la ufundi la Simba ni Selemani Matola (msaidizi), kocha wa viungo Adel Zrane, Maneja Patrick Rweyemamu, madaktari Yassin Gembe na Paul Gomez pamoja na mtunza vifaa Khamis Mtambo.

Akizungumza na Mwanaspoti bosi mmoja wa Simba, ambaye hakupenda kutajwa jina gazetini, alidai kuwa Sven amekuwa akifanya majukumu ambayo si yake ikiwamo kupanga ratiba ya mazoezi, kuingia kambini, kusafiri na masuala mengine ambayo kiutawala yanatakiwa kufanywa na Rweyemamu, ambaye ni meneja.

“Sven katika kikao cha maandalizi ya mechi hataki msaidizi wake yoyote aingie zaidi ya Matola, ambaye naye hakuna jambo analoweza kufanya zaidi ya kusikiliza tu. Matola kwa sasa hapewi nafasi ya kufanya uamuzi kuhusu masuala ya kiufundi, jambo ambalo linaleta madhara makubwa.

“Hata katika mechi wakati wa mapumziko hataki maofisa wengine kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo….anataka awepo Matola tu.

“Matola si kama akiingia katika vyumba vya kubadilishia nguo anapewa nafasi ya kushauri lolote bali anasikiliza kama ambavyo wanafanya wachezaji na baada hapo hurudi uwanjani na jambo hili hufanyika hadi mazoezini,” alisema bosi huyo na kuongeza: “Hata kwenye fainali ya Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar, Matola aliandaa kikosi cha kwanza lakini, baadaye Sven akaja kubadilisha na kupanga wengine. Hakuwapo mazoezini kwa muda wa siku mbili na alirejea siku ya fainali na kuvuruga mambo na mwisho wa siku tukapigwa”.

Ikumbukwe baada ya kupoteza mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar kwa bao 1-0, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ alitangaza kujiuzulu wadhifa huo kabla ya baadaye kubadili uamuzi wake.

Kwa mujibu wa bosi huyo, Sven hana maisha marefu ndani ya Simba kutokana na mambo yanayoendelea.

“Kiujumla hali si shwari katika benchi la ufundi kwa sababu kuna mgawanyiko wa chini kwa chini ambao hauwezi kutupa matokeo mazuri…sina uhakika sana kama huyu Sven atafika hadi mwishoni mwa msimu,” alisema kiongozi huyo.

 

ALIVYOTUA BONGO

Uongozi wa Simba mara baada ya kuachana na Aussems, waliingia sokoni kutafuta kocha mwingine na jukumu hilo aliachiwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Senzo Mazingisa ambaye licha ya kuwa na orodha ya makocha wengi waliomba nafasi hiyo alimpitisha Sven na kupeleka jina lake katika kikao cha bodi.

Mwanaspoti linafahamu viongozi wengi wa bodi walimpinga Sven kutokana na wasifu wake kwenda kinyume cha matarajio na ahadi zilizotolewa na Mo ya kushusha kocha mwenye wasifu wa maana.

Hata hivyo, Senzo alishauri kuchukuliwa kwa Sven akiamini kwa uwezo atasaidia kuijenga Simba kulingana na mbinu na umri wake.

WASIKIE HAWA

Mwanaspoti baada ya kupata taarifa hizo lilimtafuta Sven, mara baada ya mchezo wao wa kombe la FA dhidi ya Mwadui FC, ambapo alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa, muda wa kujibu maswali ulikuwa umemalizika.

Mwanaspoti liliwasiliana na Senzo, lakini jitihada hizo hazikuweza kuzaa matunda kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila majibu.