Yanga, Prisons mechi ya kufa kupona Taifa

Dar es Salaam. Yanga inaonekana kubebwa na rekodi inapoikabili Prisons katika mchezo wa kuwania Kombe la Shirikisho (FA), utakaofanyika leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ambayo msimu uliopita ilitolewa kwenye nusu fainali ya mashindano hayo na Lipuli FC ya Iringa kwa kufungwa bao 1-0, msimu huu imepania kufika hadi fainali na kuchukua kombe.

Hata hivyo, Prisons ambayo ni kama imevurugwa kwenye Ligi Kuu Bara kutokana na kufanya vibaya katika mechi tatu mfululizo, inatakiwa kukomaa kama kweli inataka kupata matokeo mazuri mbele ya wababe hao wa Jangwani.

Tangu Yanga ilipoichapa Prisons bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliofanyika Desemba 27, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Samora mjini Iringa na kuharibu rekodi ya timu hiyo kutopoteza mechi 12 tangu kuanza kwa msimu huu wa ligi, maafande hao ni kama wamepoteana kwani mechi tatu zilizofuata ilipoteza mbili dhidi ya Coastal Union na Namungo FC kisha ikatoka suluhu mchezo mmoja dhidi ya Ndanda FC.

Ushindi wa mabao 3-1 ambao Yanga iliupata kwa Singida United, wiki hii, umerejesha ari na morali katika kikosi hicho.

Timu hiyo imeonekana kuionea Prisons kila inapocheza jijini Dar es Salama kwani tangu 2009 haijawahi kupoteza mbele yake katika michezo iliyocheza na maafande hao.

Tangu mwaka huo timu hizo zimekutana mara nane jijini humo kwenye Ligi Kuu Bara na Yanga kushinda mechi saba, huku zikitoka sare mechi moja, hivyo rekodi hiyo inaonekana kuwabeba mabingwa hao wa kihistoria katika mchezo wa leo.

Katika msimu wa 2010/2011 na 2011/ 2012 timu hizo hazikukutana kwenye ligi baada ya Prisons kushuka daraja.

Hata hivvyo, kwenye mechi nane ambazo wamekutana Prisons imeifunga Yanga mabao sita huku ikiruhusu mabao 22 kutoka kwa watoto hao wa Jangwani, ambapo kipigo kikubwa ambacho Yanga imewahi kuiangushia ni cha mabao 5-0 katika mchezo uliofanyika Machi 26, 2014.

Kuelekea mchezo wa leo, Kocha wa Prisons, Mohammed Adolph ‘Rishard’ ametamba kuwa hawatishwi na rekodi za nyuma kwani hiyo ni sawa na historia na wanachodhamiria ni ushindi.