Yanga, Singida United kazi moja

Muktasari:

  • Awamu hii timu za Tanzania Yanga, Singida United, Simba na Mbao FC zimepania kufuta uteja mbele ya Wakenya na zimeahidi kuyapa uzito mkubwa mashindano hayo tofauti na misimu iliyopita ambapo zilikuwa hazipangi vikosi kamili.

Dar es Salaam. Wakati mashindano ya SportPesa Super Cup yakifunguliwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu za Tanzania zimepania kufuta uteja wa miaka miwili mfululizo zilizokuwa nao dhidi ya timu za Kenya ambazo zimekuwa tishio katika michuano hiyo.

Hii ni mara ya tatu kwa mashindano hayo kufanyika, lakini timu za Tanzania zilishindwa kufua dafu na mara zote mbili Gor Mahia ya Kenya ndiyo ilitwaa ubingwa, baada ya kuzifunga AFC Leopards katika fainali ya mwaka 2017 na mwaka jana iliichapa Simba.

Awamu hii timu za Tanzania Yanga, Singida United, Simba na Mbao FC zimepania kufuta uteja mbele ya Wakenya na zimeahidi kuyapa uzito mkubwa mashindano hayo tofauti na misimu iliyopita ambapo zilikuwa hazipangi vikosi kamili.

“Timu yoyote inapoanza msimu wa ligi inapaswa kuwa na malengo iliyojiwekea. Sisi Yanga msimu huu tulipanga malengo matatu ambayo ni kutwaa ubingwa wa Ligi, Kombe la Azam Federation Cup na hili la SportPesa, hivyo nitapanga kikosi kamili kesho (leo).

“Nimewaambia wachezaji wangu tunahitajika angalau kucheza mechi tatu kwenye haya mashindano ya SportPesa ambayo naamini ni sehemu ya kuwafurahisha Wanayanga,” alisema Zahera.

Kauli ya Zahera, iliungwa mkono na nahodha Ibrahim Ajibu ambaye alisema awamu hii hawatakuwa tayari kuona Kombe la SportPesa linakwenda nje ya ardhi ya Tanzania.

“Awamu mbili tulizoshiriki hatukufanya vizuri kwasababu tulikuwa tunacheza bila ya kuwa na kikosi kamili, lakini kwa sasa ni tofauti kidogo kwa sababu tunacheza tukiwa tumekamilika pia tuna kocha mpya,” alisema Ajibu.

Nahodha wa Singida United, Nizar Khalfan alisema baada ya ushiriki wa miaka miwili iliyopita bila mafanikio, safari hii wamejiandaa kuhakikisha wanatwaa ubingwa huo,” alisema kiungo huyo nguli.

Mratibu wa Mbao FC, Masalida Zephania alisema ingawa wanashiriki kwa mara ya kwanza, hawatakuwa tayari kuwa wasindikizaji.

Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema timu za Tanzania zimempa ahadi ya kuleta heshima huku akizitaka zitumie vikosi vya kwanza.

Mechi ya ufunguzi Singida United dhidi ya Bandari FC Yanga na Kariobangi Sharks.

Kesho pia kutakuwa na mechi mbili baina ya Mbao FC na Gor Mahia huku mechi ya jioni ikiwa ni kati ya Simba na AFC Leopards.

Bingwa wa mashindano hayo atavuna kitita cha Dola 30,000, mshindi wa pili Dola 20,000 huku mshindi wa tatu akizoa Dola 10,000.