Yanga wapewa tano maamuzi ya haraka sakata la GSM

Muktasari:

Uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti Mshindo Msolla uliingia madarakani Mei 5, 2019 wakiikuta klabu ikiwa kwenye hali mbaya kiuchumi kutokana na aliyekuwa Mwenyekiti na mfadhili mkuu, bilionea Yusuf Manji kujiuzulu mwaka 2017.

UONGOZI wa Klabu ya Yanga chini ya Mwenyekiti wake Mshindo Msola, umepongezwa kwa maamuzi ya haraka juu ya sakata ya GSM.
Kampuni ya GSM ambayo ni moja ya wadhamini wa Yanga, Machi 24 waliandika barua ya kujitoa katika baadhi ya majukumu aliyokuwa akijitolea nje ya mkataba wake kutokana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Utendaji kuingilia majukumu hayo.
Baada ya sakata hilo, viongozi wa matawi ya Klabu hiyo walikusanyika Makao Makuu ya Klabu hiyo na kutoa tamko kali la kumtaka Dk. Msolla kuwachukulia hatua wajumbe hao kabla ya kushinikiza mkutano Mkuu wa dharura.
Hata hivyo jana jioni baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, Dk Msolla alitoa taarifa ya kujiuzulu kwa wajumbe watatu, Rodgers Gumbo, Shija Richard na Said Kambi, huku Frank Kamugisha na Salim Rupia wakisimamishwa kutokana na sakata hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti mratibu wa Matawi ya Klabu hiyo Kais Edwin amesema, wao walitoa ombi na wanashukuru uongozi umelifanyia kazi haraka iwezekanavyo kwa manufaa ya Klabu ya Yanga.
Alisema, Msola kaonyesha ukomavu katika uongozi kwa kuwachukulia hatua wahusika hao huku wengine wakitakiwa kujiudhuru kuachia nafasi hizo.
"Tulisema kwa kumaanisha, ila Msolla kiongozi msikivu, kalifanyia kazi sasa tunamuomba GSM arejeshe moyo wake nyuma na kuendelea kuisapoti Yanga, haya yamepita arejee kama alivyokuwa akifanya," amesema Kais.
Juzi na jana Kamati ya Utendaji ya Yanga ilijifungia nje ya ofisi za Klabu hiyo siku mbili mfululizo kujadili sakata hilo na ndipo jana jioni ikatoka na maazimio ya kuwasimamisha wajumbe wawili huku watatu wakitangaza kujiudhuru wenyewe.