Yanga yaichakaza Prisons kuivaa Gwambina 16 bora

Dar es Salaam. Yanga imetinga hatua 16 bora ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) kwa kuichapa Tanzania Prisons kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Bao la penalti ya Bernard Morrison, pamoja na Yikpe Gnamien yametosha kuifanya Yanga kuungana na Simba, Ndanda, Sahare FC, Alliance, Gwambina katika hatua ya 16 bora.
Yanga sasa watakutana na Gwambina FC ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) katika hatua ya 16, ambayo jana Jumamosi kuichapa Ruvu Shooting kwa mikwaju ya penalti 7-6 kutokana na dakika 90 kumalizika kwa sare ya bao 1-1.
Ikicheza mbele ya mashabiki wachache waliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa, Yanga ilipata wakati mgumu kutokana na ushindani mkali ulionyeshwa na Prisons.
Yanga ilipata bao hilo katika dakika 10, kwa mkwaju wa penalti ya Morrison baada ya beki wa Prisons Michael Isamail kuunawa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi wa mchezo huo, Athuman Lazi kutoka Morogoro kuamua adhabu hiyo.
Prisons ilijaribu kubadilika kufanya mashambuliazi yake kupitia mshambuliaji wake Jeremiah Juma, lakini safu ya ulinzi ya Yanga ikiongozwa na Lamine Moro ilionekana kuwa imara zaidi.
Dakika ya 30, David Molinga alikosa nafasi ya wazi ya kuipa bao la pili timu yake baada ya piga nikupige langoni mwa Prisoni na dakika tano baadaye, Salum Kimenya naye alifanya jaribio la mbali ambalo shuti lake liligonga mwamba nakutoka nje ya lango la Yanga.
Makocha wa timu zote, Mohammed Rishard 'Adolf' wa Prisons pamoja na Luc Eymael (Yanga) walionekana kulalamikia uamuzi wa mwamuzi huyo kila wakati kwa kurusha mikono yao kuashiria hakubaliani na kinachifanyika dhidi ya timu zao.
Katika kipindi cha pili kocha Eymael alimtoa Molinga na kumuingiza Yikpe mabadiliko yaliyozaa matunda kwa Yanga kwa mshambuliaji huyo wa Ivory Coast kufunga bao la pili kwa kichwa akiunganisha mpira wa juu uliopigwa na Haruna Niyonzima.
Baada ya bao hilo, kocha wa Prisons, Mohammed Rishard 'Adolf' alimtoa, Salum Kimenya na nafasi yake kuchukuliwa na Samson Mbangula, lakini mabadiliko hayo hayakusaidia kitu kwani wapinzani wao waliendelea kutawala mchezo.