Yanga yaichapa Singida United, Azam yaua Mwadui

Singida. Yanga imeichapa Singida United kwa mabao 3-1 kwenye Uwanja Liti, Singida, huku Azam ikitandika Mwadui kwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Mabao ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji David Molinga dakika 12 kabla ya Haruna Niyonzima kupachika bao la pili dakika 50, huku Yikpe Gislain Gnamien aliyeingia akitokea benchi alifunga bao la tatu dakika 77, wakati Six Mwakasega alifunga bao la kufutia machozi kwa Singida United dakika 83. Katika kuonyesha furaha yake kocha Luc Eymael aliyepewa onyo kali na bodi ya ligi kutokana na kauli yake ya kudai kubagulia alishangilia bao la Molinga kwa kuonyesha ishara ya msalaba na kugongeana na wenzake katika benchi. Katika mchezo huo uamuzi wa Eymael kuwaanzisha washambuliaji wawili Molinga na Benard Morrison yalizaa matunda kwa mabingwa hao mara 27, kutawala vizuri mechi hiyo. Mshambuliaji Morrison alionyesha kiwango bora katika mchezo akitengeza bao la kwanza baada ya pasi yake kumkuta Mapinduzi Balama aliyempenyezea Molinga ambaye aliumalizia mpira wavuni. Katika kipindi cha pili Morrison alimtoka beki wa Singida United na kupiga krosi ya chini iliyomkuta Niyonzima aliyepiga shuti na kujaa wavuni. Yanga iliendelea kutawala mchezo huo, wakitumia kasi ya Morrison kufanya mashambulizi yao jambo lililowapa wakati mgumu wenyeji Singida United. Kocha wa Yanga, Eymael alimtoa Molinga aliyekuwa akichechemea na kumwingiza Yikpe Gislain Gnamien mabadiliko yaliyokuwa na faida kwao. Mshambuliaji Yikpe raia wa Ivory Coast alifunga bao lake la kwanza tangu ajiunge na Yanga akiunganisha kwa kichwa krosi ya Mapinduzi katika dakika 77. Wenyeji Singida United ilipata bao la kufutia machozi katika dakika 83, baada ya krosi ya Athuman Idd ‘Chuji’ kuunganishwa vizuri kwa kichwa na Six Mwakasega. Katika mchezo mwingi wa Ligi Kuu uliochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage, Azam FC imefanikiwa kuondoka na pointi tatu baada ya kuwachapa Mwadui kwa bao 1-0. Mshambuliaji Shaaban Chilunda alifunga bao pekee la Azam katika dakika 21, na kuwasongeza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi. Vikosi; Singida United: Owen Chaima, Aaron Lulambo, Haji Mwinyi, Daud Mbweni, Tumba Lui, Erick Mambo, Kazungu Mashauri, George Sangija, Elnyesya Sumbi, Haruna Moshi 'Boban' na Six Mwakasega. Yanga; Mechata Mnata, Juma Abdul, Jafary Mohammed, Lamine Moro, Saidi Makapu, Pappy Tshishimbi, Deus Kaseke, Haruna Niyonzima, David Molinga, Bernard Morrison na Balama Mapinduzi.