Yanga yaifuata Rollers, Zahera ageuka mbogo

Arusha. Licha ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya AFC Leopards ya Kenya, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema hakuridhishwa na maandalizi ya mechi mbili ilizocheza timu hiyo hivi karibuni.

Kabla ya jana kuvaana na AFC Leopards kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Yanga ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Polisi Tanzania mkoani Kilimanjaro.

Yanga iliondoka saa chache baada ya kumalizika mchezo huo kwenda Gaborone, Botswana kurudiana na Towship Rollers.

Bao la nahodha Papy Tshishimbi alilofunga dakika ya 82 kwa mpira wa kichwa uliotokana na kona ya Patrick Sibomana, halikumziba mdomo Zahera ambaye alionekana kukerwa na maandalizi duni ya mechi hizo mbili.

Akizungumza jana, Zahera alisema mechi hizo hazikuwa na maana kwa maandalizi ya mechi ijayo ya marudianoa ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rollers.

Alisema wachezaji wake hawakupata mafunzo katika mechi hizo kwa kuwa viwanja vyote viwili kikiwemo cha Ushirika, Moshi havikuwa na ubora.

“Hakuna lolote ambalo tumepata katika mechi mbili, viwanja vibovu na kule Moshi mchezaji wangu mmoja ameumia. Huwezi kusema unajiandaa kwa mechi ya mashindano halafu unacheza kwenye viwanja hivi,” alisema Zahera.

Hata hivyo, alisema hajakata tamaa ya kupata matokeo mazuri jijini Gaborone, Botswana katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Jumamosi wiki hii.

“Naamini nikienda kule kuna viwanja vizuri nitacheza kwa ufanisi, siku zote siwezi kuandaa mipango mizuri katika viwanja vibovu. Nasema tukiwa Botswana tutacheza mpira wa kiufundi kulinganisha na hapa,”alisema Zahera.

Yanga imeondoka leo alfajiri kwenda Gaborone, Botswana kuikabili Rollers baada ya kutoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Mwenyekiti wa Yanga Yanga Dk Mshindo Msolla alisema timu hiyo itapitia Nairobi, Kenya kabla ya kuwasili Afrika Kusini na baadaye itasafiri kwa basi hadi Gaborone.

“Uongozi na benchi la ufundi tumefanya maandalizi mazuri kuhakikisha tunapata matokeo katika mchezo wa marudiano,” alisema Msolla.

Mwenyekiti huyo alisema baadhi ya viongozi walitangulia Botswana kuweka mazingira mazuri na mapokezi ya timu itakapowasili huko.