Yanga yainyuka Mbao yaisubiri Pyramids

Tuesday October 22 2019

 

By Saddam Sadick

Mwanza. Bao la mshambuliaji Sydney Urikhob limetosha kuipa Yanga ushindi 1-0 dhidi ya Mbao FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Ushindi huo unaiweka Yanga katika nafasi nzuri kabla ya mchezo wake wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Pyramids ya Misri utakaofanyika Jumapili ijayo kwenye uwanja huo.
Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisema amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi katika mchezo ujao dhidi Pyramids akiahidi kufanya vizuri.
“Tulitegeneza nafasi nyingi na kuitumia moja kufunga katika mchezo huu, lakini naamini katika mchezo ujao tutakuwa vizuri na kupata matokeo, hivyo mashabiki wajitokeze,” alisema Tshishimbi.
Katika mchezo huo timu hizo zilitandaza kandanda safi, lakini washambuliaji walikosa umakini katika umaliziaji.
Ulikhob alifunga bao hilo katika dakika 55 kutokana na shuti la Mapinduzi Balama kuwababatiza mabeki wa Mbao na kumkuta mfungaji huyo na kuamsha shangwe kwa mashabiki wake waliokuwa wamejitokeza uwanjani hapo.
Kiungo Yanga, Tshishimbi hakuonyesha makeke kutokana na mipira yake kutokuwa na faida zaidi kwani pasi nyingi alishindwa kuzitumia sawasawa.
Mbao waliocheza kwa utulivu, walipata bao kupitia kwa Said Khamis, lakini mwamuzi wa pembeni, Soud Hussein alinyosha kibendera kuashiria mfungaji kuotea ikiwa dakika ya 32.
Yanga ilifanya shambulizi na kupata bao kupitia kwa David Molinga, lakini naye alijikuta kibendera cha mwamuzi wa pembeni Athuman Rajabu kimenyooshwa kuashiria kuotea.
Wachezaji wa Mbao, Yusuph Athuman na Said Khamis wameonyeshwa njano kwa kuwachezea rafu Mapinduzi Balama na Ally Ally wa Yanga.

Advertisement