Yanga yaipa jeuri Simba

Muktasari:

  • Timu za Tanzania zimekuwa hazifanyi vizuri kwenye mashindano hayo ambapo mara mbili zilizopita, ubingwa ulichukuliwa na Gor Mahia ya Kenya

Dar es Salaam. Kipigo cha mabao 3-2 kutoka kwa Kariobangi Sharks ya Kenya sio tu kimeipa kazi kubwa Simba kuhakikisha ubingwa wa mashindano hayo unabaki kwenye ardhi ya nyumbani bali pia kimewapunguzia presha ambayo wangeweza kuwa nayo iwapo wangekutana na watani wao hatua za mbele.

Baada ya mwanzo mbaya wa timu za Tanzania jana ambapo Yanga na Singida United zilijikuta zikipoteza mechi na kuondolewa mashindanoni, jicho la wadau wa soka nchini limeelekezwa kwa timu mbili za Mbao FC na Simba ambazo zinatupa karata zao leo.

Hata hivyo mchezo wa pili jioni leo unaozikutanisha Simba na Leopards ndio unaosubiriwa kwa hamu na wadau wa soka nchini kwani timu hiyo inayonolewa na Mbelgiji Patrick Aussems ndio inayoonekana yenye nguvu na misuli ya kuweza kupambana na Wakenya ambao wamekuwa wakiyapania mashindano hayo.

Ubora wa kikosi cha Simba kilichopo kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika na rekodi yake ya mechi zilizopita za kimataifa ambazo imecheza kwenye uwanja wa Taifa, ni wazi kwamba zinawapa matumaini makubwa mashabiki wake na Watanzania kwa ujumla kuwatoa kimasomaso kwenye mashindano hayo kwa kutwaa ubingwa.

Mambo hayo mawili yanaifanya Simba ipewe nafasi kubwa ya kufika mbali kwenye mashindano hayo kulinganisha na Mbao FC itakayotangulia kwa kucheza na Gor Mahia leo saa nane mchana, kutokana na timu hiyo ya jijini Mwanza kutokuwa na uzoefu wa kutosha kulinganisha na wapinzani wao ambao wametoka kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika huku wakiwa wametwaa ubingwa wa mashindano ya SportPesa mara mbili.

Lakini pia kutolewa kwa Yanga kunaifanya Simba iingine kwenye mechi ya leo ikiwa haina presha kubwa ya kukutana na watani wao wa jadi na kulazimika kutumia nguvu kubwa katika kipindi hiki ikiwa inakabiliwa na idadi kubwa ya mechi mfululizo za mashindano hayo, Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo Simba inapaswa kuwa makini na Leopards kwani timu hiyo ya Kenya imekuwa ikicheza soka la nidhamu ya hali ya juu ambalo limekuwa likizipa shida timu pinzani pindi zinapocheza nayo. Ni mchezo ambao safu ya ulinzi ya Simba inapaswa kumchunga vilivyo mshambuliaji Marcel Kaheza ambaye ni mchezaji wao anayecheza kwa mkopo kwenye kikosi cha AFC Leopards.

Kwa namna yoyote ile Simba wanapaswa kuingia kwa tahadhari kubwa na kuwapa heshima Leopards kwani timu za Kenya zimekuwa zikipania vilivyo mashindano hayo na hilo linathibitishwa na nahodha wa Leopards, Robinson Kamura “Tunajua Simba ina mashabiki wengi lakini hata sisi tunao wengi kwetu na tumeshazoea presha hivyo hatuwezi kupata shida katika mchezo huo.”

“Watarajie mchezo wa ushindani kwani malengo yetu ni kutwaa ubingwa na kwenda England kucheza na Everton,” alisema Kamura.

Kwenye mechi ya Yanga, mabao mawili ya Abuya Duke na lile la Abege George yalitosha kuifanya Kariobangi Sharks kuwazamisha vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuwatupa nje ya mashindano hayo licha ya juhudi kubwa iliyofanywa na mshambuliaji Amissi Tambwe kufunga mabao mawili.