Yanga yaishusha Simba kileleni ikiifunga Ruvu Shooting bao 1-0

Tuesday May 14 2019

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam. Tmu ya Yanga imeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa leo Jumanne Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Bao pekee la Yanga  lilifungwa na kiungo wa Yanga,Papy Kabamba Tshishimbi dakika ya 15 baada ya kutengewa pasi nzuri na Deus Kaseke lilitosha kuamsha ari ya mchezo kwa timu hiyo, tofauti na dakika 10 za mwanzo wa mchezo.

Ushindi huo wa Yanga umewawezesha kufikisha pointi 83 wakiwashusha watani zao Simba wenye alama 82 hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Baada ya mchezo huo dhidi ya Ruvu Shooting, Yanga imebakiwa na mechi mbili mkononi huku Simba ikiwa na mechi tano.

Ruvu Shooting walijaribu kufanya mashambulizi ya kusawazisha bao hilo kupitia kwa Emmanuel Martin ambaye alikuwa mchezaji wa zamani wa Yanga, lakini mashuti yake yaliishia kwenye miguu ya mwa gorikipa, Klaus Kindoki.

Kwa upande wa Yanga nao hawakuwa nyuma ambapo Heritier Makambo alipaisha mashuti mara mbili akiwa ndani ya 18.

Dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza mabeki wa kati Abdallah Shaibu 'Ninja' na Kelvin Yondan walijikuta wakilimwa kadi ya njano kwa pamoja kwa makosa tofauti.

Ninja alipewa kadi hiyo baada ya kumchezea rafu straika Ruvu, Emmanuel Martin aliyekuwa kwenye harakati za kupeleka mashambulizi kwenye lango lao, huku Yondan akapata adhabu hiyo kwa kosa la kuupigiza mpira chini kwa hasira.

Advertisement