Yanga yaitisha mkutano kujadili marekebisho ya katiba

Muktasari:

  • Uongozi wa Yanga uliingia madarakani mnamo Mei 5, 2019 ambapo Dk Mshindo Msolla alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa klabu hiyo na kuhaidi kufanyia marekebisho katiba ya klabu hiyo.

Dar es Salaam. Uongozi wa klabu ya Yanga umeitisha mkutano mkuu wa dharura wa klabu hiyo kwa lengo la kujadili marekebisho ya katiba ya klabu hiyo utafanyika Jumapili, Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na klabu hiyo leo, mkutano huo umeitishwa kwa kuzingatia ibara ya 22 ya katiba ya Yanga ya mwaka 2010.

Mkutano huo umepangwa kufanyika katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Kambarage Nyerere kilichopo Posta jijini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya agenda sita zitajadiliwa katika mkutano huo ambazo ni ufunguzi aa mkutano, kuthibitisha akidi ya mkutano, kupitisha agenda ya mkutano na kuwasilisha na kuainisha mapendekezo ya katiba (ilivyo sasa na mapendekezo mapya).

Agenda ya nne itakuwa ni kupigia kura mapendekezo ya marekebisho ya katiba na ile ya mwisho itakuwa ni kufunga mkutano.

Mapema wakati anaingia madarakani Dk Msolla kwa kutambua kiu ya mabadiliko ambayo wanachama wa Yanga wanayo, wadau mbalimbali wa klabu hiyo wameonekana kutilia mkazo suala hilo wakiamini litaleta tija kwa timu.

“Nimekuwa nikisikia mabadiliko tangu mwaka 2006, nini kinakwamisha? Nadhani viongozi waliopita pamoja na kazi kubwa waliyokuwa wakifanya, walikuwa wakijisahau kwenye hilo.

 “Nitaanza na hilo na imani yangu ni kwamba tutalimaliza kwa ushirikiano na viongozi wenzangu pamoja na wanachama wenyewe,” anasema Dk Msolla.

Katika hotuba yake kwa wanachama kabla ya mchakato wa uchaguzi kuanza, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la Yanga, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika aliutaka uongozi mpya utakaochaguliwa, kuhakikisha mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo unafanyika haraka kutokana na mahitaji ya klabu.

“Tumepitia kipindi kigumu, tuliachiwa timu, Baraza la Wadhamini, tumesakamwa lakini yote yanaelekea ukingoni.

“Tunahitaji mabadiliko yafanyike ndani ya miezi sita baada ya uchaguzi, huo ndio mkakati,” alisema Waziri George Mkuchika ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini.

Sababu zinazoilazimisha Yanga kubadili mfumo wa uendeshaji wake kutoka ule wa kawaida uliodumu kwa muda mrefu na kuingia kwenye uwekezaji.

Katiba ya Yanga

Kubadili mfumo wa uendeshaji wa klabu ya Yanga na kuingia kwenye uwekezaji ni suala lililomo kwenye katiba ya klabu hiyo ya mwaka 2010 lakini tangu mwaka 2007, Wanayanga walisharuhusu kuingia kwenye uwekezaji kama inavyoainisha ibara ya 56 ya katiba ya Yanga.

  1. “Kutakuwa na Kampuni itakayojulikana kama ‘Young Africans Sports Corpration Limited’ ambayo itasajiliwa chini ya Sheria ya makampuni kama Kampuni ya Umma yenye hisa (“kampuni”),
  2. . Wanachama wote wa klabu ambao katika tarehe ya marekebisho ya katiba ya mwaka 2007 wako hai watakuwa kwa nguvu ya uanachama wao, wanahisa katika kampuni kwa kiwango cha idadi ya hisa watakazopata kwa mujibu wa mwafaka wa Yanga uliofikiwa na Wanayanga Juni 22, 2006.
  3.  Klabu itamiliki hisa zilizo sawa na asilimia 51 ya hisa zote zilizomo katika kampuni.
  4. Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utachagua wanachama wawili ambao sio miongoni mwa viongozi wa klabu kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuwakilisha maslahi ya klabu kwenye kampuni.
  5.  Kampuni itakuwa chombo maalumu cha klabu kitakachokuwa na dhamana ya kufanya biashara ambazo klabu ya ‘Young Africans Sports Club’ itaona kuwa inafaa kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi,” inafafanua Katiba ya Yanga.