VIDEO: Yanga yaiweka pabaya Ruvu

Dar es Salaam. Bao la mchezaji wa kiungo Papy Tshishimbi, limeiweka Ruvu Shooting katika mazingira magumu ya kubaki katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Pia bao hilo limeirejesha Yanga katika uongozi wa Ligi Kuu baada ya kufikisha pointi 83, baada ya kucheza mechi 36. Simba ina pointi 82 katika mechi 33 ilizocheza.

Azam yenye pointi 69 baada ya kutoka suluhu na Simba juzi, imejiondoa katika mbio za kuwania ubingwa huo msimu huu. Matokeo mengine ya jana yameiweka Biashara United katika nafasi finyu ya kubaki Ligi Kuu baada ya kulazimishwa sare ya mabao 3-3 na Mbao FC.

Yanga jana ilirejesha matumaini ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, baada ya kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiweka Ruvu Shooting katika presha kubwa ya kubaki Ligi Kuu msimu ujao ingawa nyuma yake kuna kundi kubwa la timu zinazopambana kujinasua na janga la kuteremka daraja.

Ikiwa na pointi 42 nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi, Ruvu Shooting inabebwa na timu za Alliance yenye pointi 41, Stand United (41), JKT Tanzania (41), Biashara United (40), Mwadui (38) na African Lyon (22).

Tofauti ndogo ya pointi baina ya timu hizo haitoi nafasi kwa Ruvu Shooting kujihakikishia kubaki kwenye ligi hiyo licha ya kubakiwa na mechi mbili mkononi.

Yanga jana ilianza kwa kuwatumia mabeki wa pembeni, Juma Abdul na Haji Mwinyi kupeleka mashambulizi langoni mwa Ruvu Shooting huku wapinzani wao wakitumia mipira mirefu.

Juhudi za Yanga zilizaa matunda dakika ya 18 baada ya Tshishimbi kufunga bao. Kiungo huyo alifunga kwa shuti baada ya kupenyezewa pasi na winga Deus Kaseke.

Dakika ya 24 winga wa Ruvu Shooting, Emmanuel Martin alipiga kiki iliyombabatiza beki wa Yanga Kelvin Yondani kabla ya kipa Klaus Kindoki kudaka.

Nyota wa Yanga Herieter Makambo nusura afunge bao dakika ya 31 baada ya kupiga kiki kali iliyogonga mwamba kufuatia pasi ya Rafael Daud aliyewahadaa mabeki wa Ruvu Shooting. Makambo alitaka tena kufunga dakika ya 41, lakini kipa wa Ruvu Shooting, Rashid Abdallah aliokoa.

Kipindi cha Pili Shooting nao ilipeleka mashambulizi kwa mipango. Dakika 49 ilimtoa Zuberi Dabi na kuingia Hamisi Mcha . Dakika ya 57 Yanga ilimtoa Juma Abdul na kuingia Ibrahim Ajibu, mabadiliko ambayo hayakuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji.

Winga wa Ruvu Shooting, William Patrick nusura afunge bao dakika ya 60 kwani alipiga krosi ambayo Kindoki aliokoa kwa miguu kabla ya mabeki kuokoa hatari hiyo.

Ruvu Shooting: Abdallah Rashid, George Amani, Edward Manyama,Santos Mazengo,Tumba Sued, Zeberi Dabi, William Patrick, Shaban Msala, Fully zully, Baraka Mtuwi na Emmanuel Martine.

Yanga: Klaus Kindoki, Juma Abdul, Mwinyi Haji, Abdallah Haji, Kelvin Yondani, Feisal Salum, Paulo Godfrey, Raphael daud, Herieter Makambo, Papy Tshishimbi na Deus Kaseke.