Polisi Tanzania yalazimishwa sare na Yanga, mwamuzi akataa bao

Muktasari:

  • Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 40, baada ya mechi 21 na kuachwa na Simba kwa tofauti wa pointi 13, kabla ya vinara hao kushuka uwanjani leo saa 1:00 usiku dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa.

Dar es Salaam.Matumaini ya Yanga kuendelea na mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara yamezidi kudidimia baada ya kukubali kulazimishwa sare 1-1 na Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi.
Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 40, baada ya mechi 21 na kuachwa na Simba kwa tofauti wa pointi 13, kabla ya vinara hao kushuka uwanjani leo saa 1:00 usiku dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga ilikuwa ya kwanza kupata bao lililofungwa na Tariq Seif katika dakika 40, kabla ya wenyeji Polisi Tanzania kusawazisha kupitia Sixtus Sabelo katika dakika 71 na kuzifanya timu hizo kugawana pointi.
Katika mchezo huo mwamuzi msaidizi aliinyima Polisi Tanzania bao baada ya Matheo Antony kufunga kwa kichwa katika dakika 65, lakini mwamuzi alikataa akidai mfungaji alimsukumu beki wa Yanga, Jafari Mohamed lakini picha za video za marudio zilionyesha mfungaji hakumsukuma beki huyo.
Pamoja na bao la Polisi Tanzania kukataliwa na mwamuzi, lakini kipa wa Yanga, Farouk Shikalo alionekana akigombana na mabeki wake kutokana na uzembe uliozaa bao hilo.
Yanga ilitawala zaidi kipindi cha kwanza kwa kutalwa eneo la kiungo wakiwa na Haruna Niyonzima aliyerejea kikosini baada ya kupona malaria iliyomfanya akakosa mechi iliyopita dhidi ya Tanzania Prisons.
Niyonzima alishirikia vizuri na Balama Mapinduzi pamoja na nahodha Papy Tshishimbi wameifanya Yanga kucheza kwa utulivu zaidi tofauti na mchezo uliopita.
Ubora wa viungo wa Yanga ulimpa wakati mgumu kiungo wa Polisi, Baraka Majogoro kutoa pasi za mwisho kwa washambuliaji wake Matheo Antony na Marcel Kaheza.
Ubora wa safu ya kiungo ya Yanga umewarahisishia Nchimbi na Morrison kufanya kazi kubwa ya kumrisha mipira mshambuliaji wa mwisho Tariq Seif ambaye amefanikiwa kuiandikia bao la kuongoza timu yake dakika ya 40 baada ya krosi iliyochongwa na Nchimbi kupanguliwa na kipa na kumkuta Morrison ambaye alitoa pasi nzuri kwa mfungaji huyo aliyekwamisha mpira nyavuni kwa kichwa.
Polisi ilibadilika kipindi cha pili na kuanza kulisakama lango la Yanga na kufaniwa kupata bao la kusawazisha na kuwapa pointi inayowaweka vizuri katika msimamo wa Ligi Kuu.
Yanga yagoma kuingia vyumbani
Kabla ya mchezo kuanza kocha mkuu Yanga, Luc Eymael alisema sababu za wao kushindwa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kuwa ni mazingira machafu ya vyumba hivyo.
Yanga walionekana wakiwa nje ya uwanja wakiwa na viti vya kukaa ili kuweza kujiweka sawa tayari kwa mchezo sababu ikiwa ni kama ilivyoelezwa na kocha wao.
Eymael aliongeza kuwa wao walijiandaa vyema kwaajili ya mchezo, lakini hakupendezwa na mazingira ya uwanja ambayo sio rafiki kwa michezo ya Ligi Kuu.
VIKOSI
Yanga
Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jafari Mohamed, Kelvin Yondani, Lamine Moro, Papy Kabamba, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, Tariq Seif, Mapinduzi Balama na Benard Morrison.
Polisi Tanzania
Mohamed Yusufu, Willium Lucian, Yassin Mustapha, Idd Mobby, Mohamed Kassim, Pato Ngonyani, Jimmy Shoji, Baraka Majogoro, Matheo Antony, Marcel Kaheza na Sixtus Sabilo.