Yanga yamshusha straika mpya

Muktasari:

  • Tariq Seif ni mmoja wa washambuliaji waliofanya vizuri msimu uliopita akiwa na klabu ya Biashara United kabla ya kutimkia nchini Misri.

YANGA imemshusha nchini straika Tariq Seif na kesho Jumamosi huenda wakamalizana.
Mshambuliaji huyo ambaye msimu uliopita aliwika akiwa na Biashara United kabla ya  kutimkia nchini Misri amewasili jana Jumatani nchini akitokea nchini humo.
Baada ya kuwasili amepokelewa na Katibu Mkuu wa Yanga Dk David Ruhago ambapo inaonyesha kuna kila dalili ya kumalizana naye.
Endapo Tariq watamalizana huenda ukawa usajili wa kwanza wa Yanga kabla ya dirisha dogo la usajili kufunguliwa Disemba 15 mwaka huu huku pia akiwa ndio mshambuliaji wa kwanza mzawa wa timu hiyo msimu huu.
Msimu uliopita Tariq alionekana kuwa hatari kisha akatimkia Misri lakini usajili wake ulikwama kutokana na kuchelewa dirisha la usajili nchini humo.
Usajili huo utakuwa ni kama kutuliza mashabiki wa timu hiyo ambao bado wako katika wimbi la kusikia kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wao wa kigeni ambao wamekuwa wakivunja mikataba kufuatia hali ngumu ya maisha kwa kutolipwa mishahara yao.