Yanga yatua Mwanza kuwavaa Chama la Wana

Saturday January 19 2019

 

By Charles Abel,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mchezo wa ugenini dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Kambarage leo, huenda ukaifanya Yanga izidi kuiweka Simba kwenye wakati mgumu katika mechi zake za viporo kwenye Ligi Kuu kuelekea kwenye ubingwa wa ligi hiyo.

Ushindi wa Yanga kwenye mechi hiyo utatanua pengo la pointi baina yake na Simba inayotetea ubingwa kufikia pointi 23 jambo linaloweza kuwaweka watani wao wa jadi kwenye wakati mgumu wa kutwaa taji hilo kwa mara ya pili mfululizo.

Hadi inapoingia uwanjani leo hii kucheza na Stand United, Yanga ina pointi 53 ilizopata baada ya kucheza mechi huku Simba wakiwa nazo 33 zinazowaweka kwenye nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Simba yenye mechi nane za viporo hadi sasa, itazidi kuwekwa kwenye presha kubwa iwapo Yanga itaondoka na pointi tatu muhimu dhidi ya Stand United leo kwani itapaswa kuhakikisha inaibuka na ushindi kwenye mechi zake zitakazoifanya iwe na idadi sawa ya michezo na Yanga, ili pengo la pointi baina yao libakie tano.

Yanga inaingia kuikabili Stand ikiwa na jeuri ya kiwango na matokeo bora ambayo wamekuwa wakiyapata kwenye Ligi Kuu msimu huu ambapo hadi sasa hawajapoteza mchezo wowote, wakiibuka na ushindi mara 17 na kutoka sare mbili.

Kuja kwa mshambuliaji wake, Heritier Makambo na kiwango bora cha nahodha Ibrahim Ajibu ni silaha kubwa inayotegemewa na Yanga kuwamaliza Stand United wanaoshika nafasi ya 16 wakiwa na pointi 22.

Makambo ambaye alikosa mchezo uliopita dhidi ya Mwadui FC, ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye Ligi Kuu akiwa amefunga mabao 11 wakati Ajibu ndiye mchezaji aliyehusika kwenye idadi kubwa ya mabao ambayo ni 20, akifunga sita na kupiga pasi 14 za mabao.

Wakati Yanga ikiingia uwanjani huku ikiwa na muendelezo mzuri wa matokeo kwenye Ligi Kuu, wenyeji Stand United wenyewe wamekuwa hawafanyi vizuri na walipoteza mchezo wao wa mwisho ugenini dhidi ya Biashara United kwa bao 1-0 huko Mara.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema anafahamu ugumu wa pambano hilo kutokana na aina ya mpinzani wanayekutana naye lakini wamejipanga vizuri kuhakikisha wanapata ushindi.

“Kucheza dhidi ya timu iliyo chini kwenye msimamo wa ligi sio kazi rahisi na kipindi hiki kila timu inajiandaa vizuri pindi inapotaka kucheza na Yanga.

Nimewaambia wachezaji wangu kuhusu hilo na tumejiandaa vyema kuhakikisha tunapata ushindi,” alisema Zahera.

Kocha wa Stand United, Athuman Bilali alisema kuwa timu yake imejipanga kufuta makosa mbele ya Yanga.

“Mechi itakuwa ngumu kwa sababu Yanga wana timu nzuri na ndio wanaoongoza ligi. Kwa upande wetu bado hilo halitufanyi tuwaogope na tunaamini kama waamuzi watatenda haki, basi tutawashangaza,” alisema Bilali.

Mbali na mchezo huo wa Stand dhidi ya Yanga, mechi nyingine leo zitakutanisha Coastal Union na African Lyon, Singida United wataialika KMC wakati Azam FC itacheza na Mwadui FC.

Advertisement