Zahera, GSM wafunguka kurejea Makambo Yanga

Dar es Salaam. Wakati aliyewahi kuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera akisema kitakachomkwamisha Heritier Makambo kurejea Yanga ni mshahara, mkurugenzi wa Uwekezaji wa kampuni ya GSM, Saidi Hersi amefunguka kuhusu mchezaji huyo.

Makambo ambaye yupo kwenye rada za usajili wa Yanga kipindi cha dirisha kubwa amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake na klabu ya Horoya AC ya Guinea ambayo ilimnunua Yanga na kumpa mkataba wa miaka mitatu.

Licha ya ofisa habari wa Yanga, Hassan Bumbuli kuliambia gazeti hili jana kwamba wako kwenye mchakato wa kumrejesha mchezaji huyo, Zahera amesema ambacho kitawashinda Yanga ni mshahara wa kumlipa Makambo. Hata hivyo hakusema analipwa kiasi gani huko Horoya.

“Nilizungumza naye Makambo analipwa pesa nzuri Horoya, mshahara wake Guinea ni kama ambao wanalipwa wachezaji wa TP Mazembe ambao Yanga hakuupata na sina uhakika kama kuna mchezaji analipwa hivyo kwa sasa Yanga,” alisema Zahera ambaye alihusika kwa karibu kumuuza Makambo timu ya Horoya na ndiye alimleta Yanga akiwa kocha mkuu wa timu.

“Makambo kurudi Yanga na kuacha maisha mazuri Guinea sidhani kama itawezekana.” Awali, habari za ndani zilieleza kwamba mdhamini wa Yanga, GSM, ndiye anahusika na mpango wa Makambo kurejea Yanga, ingawa Hersi amesema mchakato wa usajili unafanywa na klabu na wao watashirikishwa.

“Kuhusu Makambo mchakato huo haupo, ila masuala ya usajili ni klabu inafanya na sisi tunashiriki tu kwa nafasi yetu,” alisema bosi huyo wa GSM ambayo hivi karibuni ilitishia kujiondoa kwenye baadhi ya huduma walizokuwa wakijitolea Yanga nje ya mkataba.

Nje ya mkataba wake, GSM imeisaidia Yanga kumrejesha Lamine Moro aliyekuwa akitishia kuondoka Jangwani kwa suala la masilahi, na pia imemsajili Bernard Morrison, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Adeyun Salehe.

Hata hivyo, Bumbuli alisema: “Mchakato wa kurejea Makambo unakwenda vizuri na inayosajili ni klabu ya Yanga, kama fedha zitatolewa na GSM au Sportpesa hayo ni masuala ya ndani, lakini tuko katika hatua nzuri za kumrejesha Makambo.”

Alisema tayari wameanza mazungumzo na klabu ya Horoya kwa ajili ya kumnunua mshambuliaji huyo ambaye wana Yanga wanaamini kama atarejea kikosini, basi timu hiyo itakuwa tishio msimu ujao.

Makamu mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema mchezaji ambaye kocha wao mkuu, Luc Eymael amependekeza asajiliwe kipindi hiki, basi atasajiliwa.

Licha ya Mwakalebela kutosema kama Makambo yupo kwenye mipango ya kocha huyo ambaye tayari amewasilisha ripoti yake kabla ya kwenda mapumzikoni, amesema ripoti imeanza kufanyiwa kazi kwenye kamati ya ufundi kabla ya kutua kwenye kamati ya utendaji.

“Mchezaji ambaye kocha amemtaka kwa kumtaja jina au position (nafasi anayocheza) atasajiliwa Yanga na wale aliowataka watolewe kwa mkopo au kuachwa, bila kujali ana mkataba na Yanga au la, basi wataachwa,” alisema.