Zahera: Hata bila mimi Yanga itafanya vizuri

WAKATI  mjadala wa adhabu za kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera ukiendelea kocha huyo ameibuka na kutoa tamko kwamba haoni hasara na hayupo pekee yake kwenye benchi la ufundi na waliopo watafanya vizuri.
Zahera raia wa DR Congo amefungiwa kukaa benchi mechi tatu kwa madai ya kutoa lugha ya kejeli kwa Bodi ya Ligi ikiwemo faini ya Sh 500,000 kwa kuvaa mavazi yasiyo nadhifu kinyume na kanuni za ligi wakati timu yake ilipocheza na Ruvu Shooting.
Katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja wa Uhuru, Yanga ilifungwa bao 1-0 ikiwa ni mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.
Zahera amesema kufungiwa kwake mechi tatu, siyo tatizo kwa timu yake kutokana na benchi lake lilivyo akitolea mfano alipokuwa kwenye majukumu yake ya timu ya Taifa aliiacha timu hiyo chini ya kocha msaidizi Noel Mwandila.
Amesema msaidizi wake ana uwezo mkubwa kwani alisimamia vyema mechi tano wakati ule na alifanya vizuri.
“Hakuna hasara yoyote kwani sipo pekee yangu kwenye benchi, Kocha Msaidizi Mwandila) anajua yote kwa sababu hata msimu uliopita niliondoka nikamuachia mechi tano akashinda nne na kupoteza moja dhidi ya Lipuli ambayo na mimi nilikuwapo,” alisema Zahera.
Kocha huyo ambaye yupo jijini hapa na kikosi chake wakijiandaa na mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco United, aliongeza kuwa haoni sababu gani za yeye kupewa adhabu hizo.
Alifafanua kuwa msimu uliopita zipo timu ambazo zilikuwa na mechi nyingi za viporo na kubainisha kuwa kigezo cha kuomba mechi yao na Ruvu Shooting kusogezwa mbele ndio Bodi ya Ligi imeamua kumfungia.
Alisema kuwa lazima Watanzania wafurahie mafanikio waliyonayo kwenye medani za soka kwani kuwa na idadi kubwa ya timu (nne) kushiriki michuano ya kimataifa ni heshima.
“Mimi nilihitaji wasogeze mechi ili wachezaji wapumzike kwa maslahi ya Taifa, lakini wamekuja kunifungia tu lazima Tanzania wajisifie kwa kuwa na timu nne kushiriki kimataifa”alisema na kuongeza
“Kuna nchi kubwa kama Senegal, Nigeria wana timu mbili kwenye michuano ya kimataifa lakini Tanzania hamfurahii hatua mliyonayo kwa sasa”alisema Kocha huyo.
Alisema kuwa iwapo Yanga itafuzu hatua ya makundi ni manufaa kwa timu za Tanzania kuendelea kuwa na timu nne kwenye michuano ya kimataifa hivyo lazima kila mmoja atambue hilo.
Kuhusu suala la kutekeleza kanuni ya mavazi, Zahera alishindwa kueleza chochote akisema kuwa waulizwe waliomfungia.
“Wanasema ninavyovaa nawakosea heshima, lakini hata Ulaya wanavaa hivi, kukosa heshima ni kuidharau Yanga ambayo ni timu kubwa na hata hivyo sikupewa taarifa kuhusu mavazi," alisema Kocha huyo.