Zahera: Simba hainipi presha

Dar es Salaam. Kocha Mwinyi Zahera amesema hatishwi na kasi ya Simba katika mbio za kuwania ubingwa kwa kuwa bado Yanga ina nafasi ya kutwaa taji hilo msimu huu.

Kauli ya Zahera imekuja muda mfupi baada ya Yanga kuchapwa bao 1-0 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, juzi.

Wakati Yanga ikipoteza mchezo huo, Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

Akizungumza jana, Zahera alisema Yanga ina nafasi ya kutwaa ubingwa kwa kuwa ana matumaini ya kushinda mechi zote sita zilizobaki huku akiomba dua baya kwa Simba.

Yanga ina pointi 74 na ikishinda mechi zote sita itafikisha 92 na Simba ina pointi 60, ikishinda mechi zake zote 15 zilizobaki itafikisha 105 na kutwaa ubingwa.

Zahera alisema bado wana nafasi kwa sababu wanaongoza ligi na idadi ya mechi ambazo Simba wamebakiwa nazo hazimpi presha kwa kuwa katika soka lolote linaweza kutokea.

Azam

Wakati Zahera akiamini katika soka lolote linaweza kutokea, anapaswa kuhakikisha anaifunga Azam iliyobeba matumaini ya ubingwa wa Yanga na Simba msimu huu.

Yanga ina mechi mbili dhidi ya Azam nyumbani na ugenini huku Simba nayo ikiwa na mechi moja dhidi ya timu hiyo.

Azam itacheza dhidi ya Yanga Aprili 29 na mechi nyingine itapigwa siku ya mwisho ya kufunga msimu huu wa ligi. Simba na Azam zitacheza Mei 12 baada ya Simba kushinda mabao 3-1 katika mechi ya kwanza.

Kama Yanga itapoteza mechi ijayo dhidi ya Azam basi ndio itakuwa imejiwekea nafasi ngumu ya kutwaa ubingwa msimu huu, hivyo nguvu kubwa itahamishia kwenye Kombe la Shirikisho (FA) ambako Simba ilishatolewa.

Rekodi zinaonyesha tangu mwaka 2015 timu hizo zimekutana mara sita na Yanga imeshinda mechi mbili tu, Azam imeshinda moja na zimetoka sare mara tatu. Wapinzani wao Simba wanaweza kupata wakati mgumu kwa Azam kwa sababu wana lambalamba hao hawatakubali kufungwa tena baada ya mechi ya mzunguko wa kwanza kukubali kipigo cha mabao 3-1.

Kwa upande wa Simba tangu mwaka 2015 timu hizo zimekutana mara tisa, Simba imeshinda mechi nne, sare nne. Azam imeshinda mechi moja na mara ya mwisho Azam kuifunga Simba kwenye Ligi Kuu ni Machi 30, 2014 iliposhinda mabao 2-1.

Kocha wa Azam, Abdul Mingange alisema hesabu zake zipo katika mbio za kutwaa ubingwa wa Kombe la FA kwa kuwa hawana ubavu wa kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Wakati huo huo, Azam jana ilichapwa bao 1-0 na Ndanda FC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.

Azam ipo nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 66 na Ndanda imefikisha pointi 43.