Zahera awatumia Yanga B maandalizi mechi ya Azam FC

Muktasari:

  • Yanga leo imeendelea na mazoezi katika uwanja wa Polisi Kurasini ikiwa na wachezaji wa kikosi B kuelekea mchezo dhidi ya Azam FC Jumatatu

KOCHA wa Yanga SC, Mwinyi Zahera leo amewafanyisha mazoezi wachezaji wa timu ya vijana, maarufu kama Yanga B kuelekea mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Azam FC Jumatatu, kufuatia wachezaji wa kikosi cha kwanza kuendeleza mgomo.

Kwa siku ya pili leo, wachezaji wa Yanga SC wamegoma kufanya mazoezi wakishinikiza walipwe malimbikizo ya mishahara yao pamoja na fedha za usajili.

Mgomo huo ulianza asubuhi Uwanja wa Chuo cha Maafisa wa Jeshi la Polisi, Kurasini mjini Dar es Salaam wakati wachezaji walipokutana kwa ajili ya mazoezi ya asubuhi.

Mazoezi ya kikosi B yalianza saa 2 dakika 20 na kumalizika saa nne dakika 20 wachezaji wa kikosi cha kwanza waliudhuria mazoezini lakini hawakufanya mazoezi waliishia kukaa ndani ya magari yao. Hadi mazoezi yanamalizika hakuna mchezaji hata mmoja wa kikosi cha kwanza aliweza kujumuika katika mazoezi.

Zahera alikuwa amekwishajiandaa kwa kuwaita wachezaji wa timu B na baada ya nyota wa kikosi cha kwanza kusisiza mgomo wao wa hadi wakutane na viongozi, Mkongo huyo akaendelea mazoezi na wachezaji wa timu ya vijana watupu.