Zahera ajitosa ishu ya Yondani kukataa mkono wa Ajib

Muktasari:

  • Ajib alifanya utambulisho wa kusalimia wachezaji wenzake alipokuwa anatambulisha katika mchezo wao dhidi ya Yanga, wakati nahodha anakuwa anatakiwa kutambulisha na sio kusalimia.

Dar es Salaam.Tukio la Nahodha wa Yanga, Ibrahim Ajib kukataliwa mkono na mchezaji mwenzake Kelvin Yondan, liliibua mijadala mingi kwa wachezaji hao wawili.

Mijadala hiyo ilikuwa inaeleza kwamba Yondani amegoma kumpa mkono Ajib kutokana na kuvuliwa unahodha na kocha Mwinyi Zahera, lakini kocha huyo amesema tukio hilo ni kutokana na Ajib kutokuwa na uelewa.

“Ile picha iliyokuwa ikisambaa naweza kusema kwamba Kelvin alifanya kusudi, kwa sababu kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Kelvin alimcheka Ajib na kumuambia aliwahi kuona wapi Kapteni anasalimia wachezaji wenzake,” alisema.

Zahera aliongeza kwamba baada ya tukio hilo wachezaji wenzake wote walicheka, lakini hakuna tofauti yoyote kwa wachezaji hao kama ambavyo wengi wanasema.

Yondani alikataa kumpa mkono Ajib wakati kikosi cha Yanga kilipokuwa kinatambulishwa, hali ambayo ilizua mijadala mingi nje ya uwanja.