Zahera atimuliwa akiiandaa Yanga kuifuata Ndanda

Muktasari:

Zahera leo asubuhi amefika mazoezini kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini na kuendelea na majukumu yake wakati timu yake ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda ya Mtwara.

Dar es Salaam. Yanga imevunja mkataba na kocha wake Mwinyi Zahera pamoja na benchi zima la ufundi sambamba na kuvunja kamati ya mashindano.
Zahera ametimuliwa na klabu hiyo wakati mwenyewe ameendelea na kazi yake kama kawaida.
Zahera leo asubuhi amefika mazoezini kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini na kuendelea na majukumu yake wakati timu yake ikijiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Ndanda ya Mtwara.
Winga wa Yanga, Mrisho Ngassa amethibitisha kuwa katika mazoezi yao yakisimamiwa na kocha Zahera.
Ngassa amesema Zahera hajawaambia lolote juu ya uvumi wa kupoteza kazi yake zaidi ya kuwambia leo jioni wataingia kambini tayari kwa safari ya kwenda Mtwara kuwafuata Ndanda.
Mkongwe huyo amesema baada ya kumaliza mazoezi wameona taarifa hizo ingawa hawajatangaziwa lolote juu ya mabadiliko yoyote.
Wakati Ngassa akiyasema hayo mmoja wa viongozi wa benchi la ufundi la Yanga amethibitisha kwamba viongozi wote wa benchi lao wameitwa klabuni kuanzia saa sita.