HISIA ZANGU: Zana Coulibaly na beki Ninja katika hadithi zao tofauti

ILIKUWA ngumu kumwelewa Zana Coulibaly katika siku zake za mwanzo. Alikuwa mwanasoka halafu mchekeshaji. Sikumuelewa kwa sababu sikuwahi kumuona uwanjani. Nilimuona mitandaoni kule Instagram. Nilipomuona mara ya kwanza ilikuwa fainali Kombe la Mapinduzi. Hakunishawishi sana.

Alikuwa mzito. Nilitaka kumuona Coulibaly aliye mwepesi zaidi kutokana na nafasi yake ya beki wa kulia. Sikumuona kama yuko fiti kama mtu wa nafasi yake ambaye anauguza mguu wake kwa sasa pale Msimbazi, Shomari Kapombe.

Tatizo la Coulibaly ni kwamba alikuwa anatokea kila mahala. Mchekeshaji, mkata viuno katika basi la timu. Mashabiki wa Simba wakaanza kukasirika. Alikuwa anawapa Yanga kitu cha kusema. Hakujua utani wake wa kukata viuno ulikuwa unawaudhi Simba.

Yanga ilikuwa inasema Simba imelamba garasa. Simba wenyewe wakaanza kuingia na hofu huenda wamelamba garasa kutoka Ivory Coast. Nikasikia minong’ono kwamba anaweza kukatwa nafasi yake ikachukuliwa na mtu mwingine.

Baadaye nikamuona tena Coulibaly mechi nyingine. Kisha nikamuona tena na tena. Halafu nikamuona Jumamosi. Kila siku anabadilika. Kila siku anakuwa mzuri zaidi ingawa anahitaji kukata uzito wake tena na tena. Ujinga wake wa nje ya uwanja unamfanya ajiamini zaidi na zaidi.

Sasa hivi amekuwa Coulibaly tofauti. Taratibu anaanza kuwa tegemeo la Msimbazi katika ule upande wa kulia. Juzi kawasumbua sana Yanga. Nilikuwa nacheka jinsi alivyomkalisha Abdallah Shaibu ‘Ninja’ chini wakati akitaka kupiga krosi yake moja.

Atawasaidia sana kina John Bocco na Meddie Kagere kufunga kwa sababu hana mambo mengi katika kibendera cha kona. Kila akifika anamimina krosi ili washambuliaji wafanye kazi zao. Hamu yake ni kupiga krosi na sio kuonyesha mbwembwe nyingi kwa mtu anayekabiliana naye.

Tujifunze kuwaelewa wachezaji wanapowasili nchini. Wengine wanakumbana na mazingira tofauti ambayo yanawafanya kuingia katika mfumo wa soka letu taratibu. Kuna wachezaji waliwahi kukatwa na Yanga na Simba wakati usajili ukiendelea. Kisa? Walionekana kutokuwa wazuri sana. Mechi za kirafiki za maandalizi ya msimu tu zikawaondoa. Kumbe ni wachezaji wazuri na walihitaji kuingia taratibu katika timu.

Ni kama ilivyo kwa mchezaji wa Yanga anayeitwa Ninja. Kwa sasa ni tegemeo pale Jangwani. Nimeshangaa sana. Alianza vibaya Yanga na ikaonekana kama vile Yanga imelamba garasa. Wiki iliyopita wakati alipofanya ujinga Tanga bila ya kuonyeshwa kadi nyekundu watu wa Yanga wakafanya fitina ili mradi acheze mechi ya Simba na Yanga. Ni kweli walifanikiwa.

Huyu Ninja ananikumbusha Nadir Haroub Cannavaro alivyoingia Yanga. Alikuwa anaonekana chizi. Baadaye akaja kuwa mchezaji muhimu Yanga kwa sababu mbili. Kwanza alikuwa anafanya vema kazi yake ya kulihami lango kwa kubutua na kuurudisha mpira ulikotokea.

Baadaye Cannavaro akajituliza na kuanza kujifunza kucheza kutokea nyuma. Baadaye zaidi akajitanabaisha kwamba alikuwa beki bora katika tackling nchini. Amemaliza mpira akiwa na heshima kubwa alikuwa ni bonge la beki.

Huyu Ninja anaelekea huko. Afadhali Yanga hawakukata naye tamaa wakati alipokuwa anasugua sana benchi. Lakini sasa ameanza kuwafaa. Nimemtazama jinsi alivyo na umbo kubwa na miguu mirefu. Anaweza sana kufanya tackling. Nadhani wachezaji wa Zanzibar wanajua misingi ya mpira kuliko wale wa Bara.

Ninja anacheza mipira mingi ya hewani. Anafuata njia zilezile za Nadir. Uzuri ni kwamba umri wake ni mdogo na ana muda wa kurekebishwa mapungufu yake kama vile ambavyo mashabiki wanaamini ana akili ndogo uwanjani.

Umbo lake lilivyo nadhani atakuwa anatamaniwa yeye zaidi miongoni mwa mabeki wetu kama wazungu wakija kutafuta beki. Wazungu waliwatengeneza kina Sol Campbell kuwa mabeki ingawa kiasili sio wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Kazi ya kwanza ya beki ni kulihami lango. Kina Pep Guardiola wanajaribu kutuletea aina mpya ya mpira ya mabeki kucheza mpira kama viungo wakati kiasili kazi yao ya kwanza ni kulihami lango. Huyu Ninja anaweza kufuata njia ya Cannavaro kwa kujua namna ya kulihami lango.

Akiendelea kucheza tena na tena katika kikosi cha kwanza hatimaye atajiamini zaidi na zaidi na mwisho ataanza kucheza kutokea nyuma. Nilimuona mechi ya Simba akijaribu kuanza kucheza kutokea nyuma. Ni kitu kizuri. Anaweza kuisaidia timu ya taifa siku za usoni.

Mpira wetu katika timu kubwa ni mgumu sana kwa wachezaji wapya. Hawapumui. Hawapati nafasi ya kueleweka uwezo wao na tabia zao. Ndio maana leo Hassan Dilunga ni mmoja kati ya viungo bora nchini.

Anavaa jezi nyekundu lakini kama Yanga wangemvumilia si ajabu leo ndio angekuwa mbadala wa kina Thaban Kamusoko katika jezi yao.

Tuanze kujifunza kuwaelewa wachezaji. Tuwape muda wa kuingia katika timu taratibu. Nimegundua wachezaji wana tabia tofauti ndani na nje ya uwanja.

Wengine wanachanganya taratibu zaidi hadi kuweza kuipata kasi na wengine wanaikngia kwa kasi.