Zidade ashusha presha Barca ikilala nyumbani

Muktasari:

Ingawa Barca walionyesha kuanza kuzinduka baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wiki hii, kipigo cha jana kitawapa maswali zaidi, hasa kocha wao mpya, Ronald Koeman.

Barcelona, Hispania (AFP). Real Madrid jana ilirejesha makali yake baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Barcelona katika mchezo wa Ligi ya Hispania, La Liga iliyochezwa kwenye uwanja wa Nou Camp, nyumbani kwa wapinzani.

Ingawa Barca walionyesha kuanza kuzinduka baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 katika mechi ya Ligi ya Mabingwa wiki hii, kipigo cha jana kitawapa maswali zaidi, hasa kocha wao mpya, Ronald Koeman.

Wakati Real walipoteza mechi mbili mfululizo; ya La Liga na Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, Barca ilitakiwa itumie nafasi ya jana Jumamosi kuongeza machungu kwa kumpa Zinedine Zidane kipigo cha  na kumuongezea presha.

Badala yake, ushindi wa Madrid umewafanya wawe juu ya wapinzani wao kwa tofauti ya pointi sita, wakiwa wamecheza mechi moja zaidi.

Madrid ilianaza kama ilivyotarajia wakati Karim Benzema alipokwenda kuchukua mpira upande wa kulia na akapata nafasi ya kugeuka, akimuona Valvede mbele yak akikimbia kuelekea golini.

Mfaransa huyo akamburuzia pasi na Valverde akajipa nafasi kabla ya kuachia mkwaju mkali uliojaa juu kushoto kwa kipa . 

Lakini ndani ya dakika tatu, Barcelona ilisawazisha. Messi, akitokea upande wa beki wa kushoto, aliubetua mpira juu kumpa Jordi Alba, ambaye aliukunja kwa kiki kali mbele ya lango la Real, ambako Fati akausukumia wavuni akiwa mbele ya Ramos.

Benzema angeweza kuongeza bao jingine lakini akashindwa na Madrid ikamaliza kipindi cha kwanza ikionekana imara zaidi ya wenyeji.

"Ni pointi tatu tu, lakini lazima tuzifurahie hasa baada ya mengi kusemwa kuhusu kikosi hiki," alisema Zidane.

Penati iliyopigwa na Sergio Ramos na bao lililofungwa mwishoni mwa mchezo na Luka Modric liliimaliza Barcelona baada ya Federico Valverde na Ansu Fati kuzifungia timu hizo mabao mapema katika mechi hiyo ambayo ilikwenda tofauti na wale waliokuwa wakihitaji ushahidi zaidi kwamba vigogo hao wanaporomoka.

"Mara kwa mara unakutwa na vipindi vibaya katika msimu na tunatumaini kuwa kipindi hiki kimedumu kwa wiki moja tu," alisema Ramos. "Kushinda mechi dhidi ya mpinzani wako wa muda mrefu kuliko wote ni kitu kinachoridhisha."

Barcelona inaweza kujiona imeshindwa kwa shida, hasa baada ya penati ya Ramos baada ya kufanyia uhakiki VAR na kuanguka kulikokuzwa na nahodha wa Madrid baada ya Clement Lenglet kumvuta jezi.

"Labda siku moja unaweza kuelezea VAR inafanyaje kazi hapa Hispania," alisema kocha Ronald Koeman. "Tulikuwa na mechi tano za ligi na VAR imeingilia tukio dhidi ya Barca."

Lakini ukiacha kipindi cha kwanza ambacho Lionel Messi alionyesha kutaka kuipa Barca ushindi kwa juhudi zake binafsi, Madrid ilitawala mchezo kwa vipindi virefu na kupata ushindi wakati ulipostahili.

Hii ilikuwa ni mechi ya kwanza ya Classico kwa Ronald Koeman akiwa kocha wa Barcelona na baadhi ya presha ambazo Zidane angekabiliana nazo kama angeshindwa, sasa zitahamia kwa Mholanzi huyo, ambaye ameshashinda mechi tatu tu kati ya sita alizoiongoza timu hiyo hadi sasa.

Barcelona inakutana na Juventus Jumatano katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya, bila ya Gerard Pique, ambaye anatumikia adhabu.