Zidane ataka Madrid wapambane kwa Barcelona

Friday October 23 2020
zidane pic

Madrid, Hispania. Zinedine Zidane anasema anaungwa mkono kwa asilimia mia na rais wa Real Madrid, Florentino Perez na amewataka wachezaji kuanza vizuri msimu kwa kuizamisha Barcelona leo.

Madrid na kocha wao wanaelekea Camp Nou wakiwa katika hali ngumu baada ya kupata vipigo viwili mfululizo, kwa kulazwa na Cadiz katika La Liga na baadaye Shakhtar Donetsk katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Alipoulizwa jana kama bado anajiona kuwa anaungwa mkono na rais wa klabu hiyo, Zidane alisema: "Ndio, na kila mtu. Nimeshinda vitu vingi pamoja na wachezaji hawa na nitakuwa nao wakati wote hadi kifo. Wakati wote nitakuwa nao.

"Lakini htuna budi kubadili hali yetu, tulikuwa na mechi mbili ngumu, na hipo ndipo mambo yote yalipo. Kila mara kuna wakati mbaya lakini kuna timu za aina hiyo katika nyakati hizo ambazo huonyesha tabia yao na ubora. Hatuna budi kufanya hilo kesho."

Zidane alisema Sergio Ramos atakuwepo katika mchezo huo dhidi ya Barcelona baada ya kupona goti ambalo lilimfanya akose mechi waliyopoteza dhidi ya Shakhtar Jumatano.

"Sergio ni nahodha wetu, kiongozi wetu," alisema Zidane. "Amepona, atakuwa nasi. Ni suala la kuwa timu kimwili kwa asilimia 100 na nadhani kwamba Sergio ameshafikia hapo."

Advertisement

Barcelona pia itaingia katika mechi hiyo maarufu kwa jina la El Clasico ikiwa imetoka kupata kipigo katika La Liga, ingawa walizinduka kutoka katika kipigo cha bao 1-0 mbele ya Getafe mwishoni mwa wiki iliyopita, na kuibuka na ushindi wa mabao 5-1 nyumbani dhidi ya Ferencvaros katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Jumanne.

"Kinadharia, timu zote ziko katika hali ngumu," alisema Ronald Koeman, ambaye atakuwa akiiongoza timu kwa mara ya kwanza katika mechi ya Clasico, akiwa kocha wa Barcelona.

"Labda katika wiki mbili zilizopita Madrid haijawa katika kiwango chake, lakini hilo halimaanishi kuwa ni timu mbovu.

"Ni timu kubwa, iliyo na wachezaji wazoefu, ambao wanajua kuikabili hali ngumu, na watataka zaidi ya kila mtu anayetaka ushindi baada ya kufungwa mechi mbili."

"Siitegemei Madrid inayofungika, nategemea kinyume chake," aliongeza Koeman.

Advertisement