‘Amka Ruge inakusubiri dunia’

Ruge Mutahaba.

Muktasari:

Imekuwa safari ndefu kwa familia, wafanyakazi wenzake, mashabiki ambao wameguswa na kutaka kuchangia matibabu ya tatizo la figo linalomkabili Ruge Mutahaba.

Imekuwa safari ndefu kwa familia, wafanyakazi wenzake, mashabiki ambao wameguswa na kutaka kuchangia matibabu ya tatizo la figo linalomkabili Ruge Mutahaba.

Ukimya wake umewaamsha watu mbalimbali waliomfahamu kutaka kumrudishia afya yake kwa kuchangia matibabu.

Wasanii, watu mashuhuri na wanasiasa wamejitokeza kuunga mkono juhudi za kuhakikisha michango ya hali na mali inatolewa ili kumwinua kitandani.

Juzi, Mbunge wa Mtama , Nape Nnauye aliiomba familia kuruhusu Watanzania kuchangia matibabu yake kutokana na mchango wake mkubwa katika maisha ya watu mbalimbali nchini.

Ombi la Nape alilitoa alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds TV, ambalo familia iliridhia.

Kaka wa Ruge, Mbaki Mutahaba, ametoa namba 0752 222 210 kwa ajili ya kuchangia na kutuma ujumbe mbalimbali wa kumfariji.

Mbaki anasema katika matibabu hayo kwa siku walikuwa wakitumia mpaka Sh5 milioni kulingana na hali ya mgonjwa.

Pia, anaeleza kuwa mpaka sasa wameshatumia zaidi ya Sh650 milioni kwa ajili ya matibabu ya mdogo wao huku Sh530 milioni zikitolewa na kampuni ya Clouds Media.

Anasema anashukuru tangu waruhusu watu kuchangia mwitikio umekuwa mkubwa, jambo ambalo kama familia wanafarijika.

Wengi wafunguka kuhusu Ruge

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais- Muungano na Mazingira, January Makamba, mbali na kumsifu alishauri kufanyika kwa tamasha litakalokusanya fedha kwa ajili ya kupata fedha za matibabu yake.

Anasema ni vizuri jambo hilo likasimamiwa na wasanii wenyewe.

Anasisitiza kuwa hapa ndipo wasanii wenye mabifu kuyaweka pembeni tofauti zao na kufanya tamasha kubwa kuliko yote yaliyowahi kutokea nchini.

Kwa kufanya hivyo, anasema ana imani Ruge atapona na kurudi katika hali yake na kuongeza kuwa wagonjwa hupata faraja wanapoona kuna watu wako nyuma yao ukiachilia mbali madaktari ambao huwahudumia.

Makamba anasema jambo hilo endapo watalichukua watu wa siasa linaweza kuleta maneno, hivyo ni vyema wasanii wenyewe wakaliratibu.

Majizzo

Mbali na Makamba pia Mkurugenzi wa kituo cha redio cha EFM na TV E, Francis Ciza maarufu kwa jina la ‘Majizzo’ ameahidi kufanya jambo katika uchangiaji wa matibabu hayo na kueleza kuwa tayari ameunda kamati ambayo itaratibu hilo.

Jana, akihojiwa katika kipindi cha 360, Majizzo anasema Watanzania watarajie kamati hiyo itafanikisha walilokusudia na kuwaomba wasiache kuwapa ushirikiano pale watakapowafuata kueleza walichoamua kufanya katika kufanikisha matibabu hayo.

“Lengo letu ni moja kuhakikisha Ruge anarudi mtaani kwani game bila yeye inakuwa haina ushindani, Watanzania tunapokuja kwenu tunaomba mtupokee, kwani Ruge ni wetu sote sio wa Clouds tu,” anasema Mkurugenzi huyo.

Akielezea uhusiano wake na Ruge, Majizzo anasema tofauti na watu wanavyofikiria kuwa wana uadui, lakini ukweli ni kwamba ana mchango mkubwa katika harakati za maisha yake na ndio maana hata Clouds walipomwita kwenye kipindi hakusita kwenda.

Majizo anabainisha kwamba Ruge mbali ya kuwa rafiki ni kaka na mshauri na kuongeza kuwa hata yeye alipofika hapo na kufungua redio na televishenui ana mchango kwake.

Anasema Ruge ni mshindani mzuri wa kibiashara na kwamba unaposhindana naye yakupasa kuwa makini kwani ni mtu mwenye kufanya mambo kwa kutumia akili.

Pamoja na ushindani wake huo, anasema anampongeza kuwa mtu wa tofauti kwani linapokuja suala la biashara na mambo binafsi huwa anaweka pembeni na kushauri vijana wa sasa kuiga mfano wao kwa kushirikiana linapokuja suala la kufanya biashara na kuweka tofauti zao pembeni.

“Mfano katika kampeni mwaka 2015, alinieleza kuwepo kwa fursa na kunishika mkono kunielekeza namna ya kuingia huko na ninashukuru nilifanikisha, hali ambayo kwa watu wengine ambao wana ushindani wa kibiashara ni ngumu kulifanya hilo,” amesema.

Wakati kuhusu suala la kufungua redio, amesema nalo lina mchango wake kwani pamoja na kukatishwa tamaa lakini alikuwa akimpa A, B,C za namna ya kulifanikisha na hata alipofanikisha alikuwa mtu wa kwanza kumpigia simu.

Majizo anasema tofauti na watu nje wanavyowachukulia kuwa ni maadui, wao ni watu wa karibu na wamekuwa wakipigiana simu hadi saa kumi usiku.

Barnaba

Msanii Elias Barnaba maarufu kwa jina la Barnaba Boy, anasema wakati amesajiliwa pale THT, alikuwa hana nauli ya kumpeleka na kumrudisha nyumbani lakini Ruge alikuwa akimpa na wakati mwingine ananisindikiza hadi kituo cha Mbuyuni kupanda daladala halafu yeye anageuza.

“Kuna siku ananifuata hadi Kigogo, alikuwa ananipenda sana....baadaye akaninunulia gitaa. akaanza kunilea kama mtoto wake, kuna kipindi sina nguo za kuvaa, Ruge akawa ananinunulia nguo au anachukua nguo zake nyumbani na kuja nazo THT asubuhi sana ananipa fuko la nguo kubwa, tunaenda kwa fundi tunazipunguza,” anaeleza Barnaba.

Mpoto

Naye Msanii wa maarufu anayefanya muziki wa kughani mashairi, Mrisho Mpoto, amesema ubunifu wa kutovaa viatu ni wa Ruge japokuwa hakutaka amtaje na kumwambia ataje sababu nyingine ila asimuhusishe.

Akielezea zaidi Mpoto anasema wakati anaanza muziki huo, Ruge alitaka awe na kitu ambacho kitamtambulisha kwa watu na kiwe tofauti.

“Tukisema rasta watu wengi wanazo, pia wazo lako la kuvaa magunia ni zuri lakini lazima uyabuni kiasi kwamba hayatakufanya watu wakuone mchafu kwa kupeleka kushona na wabunifu wa mavazi.

‘Lakini tukija kwenye viatu, je tutakuvalisha raba au viatu gani. Hivyo mwisho wa siku katika maswali yote hayo kati yangu na Ruge mwisho wa siku ikaamuliwa niwe natembea peku na ndio maana leo mnaniona natembea bila viatu,” anasema Mpoto.

Hata hivyo, anaeleza kuwa awali uimbaji wake watu wa Clouds walikuwa hawaulewi na wakati mwingine ilichukuliwa kama anaipinga Serikali, lakini Ruge alisimama na kusema ndio anautaka huohuo na kuanza kufanya naye kazi ikiwemo kuzunguka naye kwenye jukwaa la fursa ambako alikuwa mmoja wa watoa mada.

Mbali na sanaa, Mpoto anasema pia Ruge amemsaidia katika masuala ya maisha kwani ndio sababu ya yeye kumiliki shamba la heka 50 baada ya kumkatalia kununua gari pindi alipofanya na kazi na kulipwa zaidi ya Sh50 milioni na leo amekuwa msambazaji mkubwa wa matunda na mbogamboga maeneo ya mjini Jijini Dar es Salaam.