Babu Tale:Tumekoma, hatutarudia tena

Thursday January 24 2019

 

By Nasra Abdallah,Mwananachi [email protected]

Meneja wa Kampuni ya Wasafi (WCB) inayowamiliki wasanii Naseeb Abdul, maarufu kwa jina la Diamond na Raymond Mwakyusa’ Rayvanny, amesema adhabu waliokuwa wamepewa wasanii wao kwa miezi miwili, imewafundisha na hawatarudia tena.

Meneja huyo Babu Tale ambaye jina lake halisi ni Hamis Taletale, alisema hayo katika mahojiano yake na Mwananchi, ikiwa ni siku moja tangu Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), litangaze kuwafungulia wasanii hao baada ya kuwafungiwa tangu Desemba mwaka jana kutokana na sababu za kimaadili.

Baraza hilo pia, limeruhusu kuendelea kwa tamasha la Wasafi ambalo tayari lilifanyika mikoa sita hapa nchini kabla ya kulifungia baada ya wasanii hao kuimba wimbo wa Mwanza uliofungiwa wakiwa katika tamasha hilo mkoani Mwanza Desemba 15.

Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na katibu mtendaji wa baraza hilo, Godfrey Mngereza, inaeleza kuwa wamewafungulia wasanii hao kuanzia Januari 22 na kueleza kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea maombi kadhaa ya kukiri kosa na kuomba msamaha kutoka kwa wasanii hao na WCB.

“Baada ya kuyapitia maombi hayo ambayo pia yaliwasilishwa kwa mwenyekiti wa modi ya maraza na kwa kuzingatia jukumu la Basata la kusimamia, kuendeleza na kukuza wasanii na sekta ya Sanaa nchini, baraza limeamua kuwaruhusu wasanii tajwa kuendelea na shughuli za Sanaa,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo, Babu Tale alisema hawana neno kubwa isipokuwa ahsante na kuongeza kuwa wamekoma na hawatarudia.

“Kwa kweli kwa muda wote ambao wasanii wetu walifungiwa pamoja na kusitishwa kwa tamasha letu la Wasafi, tumejifunza mengi, hatuna budi kuishukuru Basata na Serikali kwa ujumla, tunachowahidi ni kwamba tumejifunza mengi na hatutarudia tena,”alisema Tale.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Diamond alishukuru uamuzi wa Basata na kueleza kuwa sanaa ni kazi, hivyo ni wajibu kuilinda, kuipenda na kuithamini.

Pia, aliompongeza Rayvanny kwa kuwa huru na kueleza kuwa ni wakati sasa wa kuachia wimbo wao mpya mwaka huu.

Rayvanny naye hakuwa nyuma, katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Mungu ni Mwema”.

Rayvanny na Diamond, walifungiwa Desemba 18 mwaka jana kutofanya maonyesho ndani na nje ya nchi kwa muda usiojulikana wakituhumiwa kufanya makosa mbalimbali tangu kuanza kwa tamasha la Wasafi.

Hata hivyo, Basata imesema licha ya kuwafungulia itaendelea kufuatilia utendaji kazi wa wasanii hao na Kampuni ya Wasafi ili kuhakikisha wanazingatia sheria na taratibu za nchi.

Advertisement