Billnass afafanua kuhusu picha yake

Thursday March 28 2019

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Baada ya kusambaa kwa picha ikimuonesha ameloana sehemu za mbele katika suruali yake, msanii William Lymo maarufu ‘Billnass’, amesema mtoto aliyekuwa naye alimmwagia maji.

Picha hiyo iliyosambaa mapema wiki hii, ilimuonyesha staa huyo akiwa katika mechi kati ya Taifa Stars na Uganda iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa, Jumapili Machi 24.

Billnass aliyekuwa amevalia suruali ya jeans iliyochanwa eneo la magotini, alionekana akiwa anajishangaa namna alivyolowana.

Watu walioiona picha hiyo kila mmoja aliitafsiri kwa namna yake huku wengine wakienda mbali na kueleza kuwa ni madhara ya kampeni ya vinywaji vya nusu bei iliyokuwa gumzo siku hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, Billnass ambaye alipata umaarufu kupitia wimbo wa ‘Chafu Pozi’, amesema kilichompata hadi kujikuta ameloa ni kumwagiwa soda na mtoto aliyekuwa naye.

“Pale mpirani nilienda na mtoto ambaye ni wa rafiki yangu, unajua tena watoto hawatuliagi sehemu moja hivyo wakati anakunywa soda akajikuta ananimwagia na kuonekana vile,” anasema msanii huyo ambaye kwa sasa anatamba na wimbo wa ‘Fungua Geti’.

Kuhusu kumuhusisha kwamba alipata mfadhaiko baada ya kumshika mtangazaji wa Clouds, Shadee, alisema hakuna ukweli wowote kwani anaheshimiana naye kama dada na kaka. Kuhusu vinywaji vya nusu bei, alisema katika maisha yake hajawahi kunywa pombe na hafikirii.

Advertisement