DJ SinyorRita ajivunia kuwa na fani ya kipekee

Kazi ya uDJ au kuchezesha santuri si kazi rahisi hasa inapofanywa na mwanamke kwani inamtaka kukesha usiku kucha kwenye kumbi za burudani.

Hata hivyo Mwanaisha Said au DJ Sinyorrita anajivunia kazi hiyo anayoiona kuwa ya kipekee akiwa miongoni mwa wanawake wachache maDJ nchini.

Akizungumzia kufanya kazi usiku kwanza anakiri kukesha usiku kumebadili utaratibu wake wa kulala, amejikuta akilala mchana. “Wakati watu wengine wanapumzika usiku, mimi hata kama sina kazi inakuwa vigumu kulala, sipati usingizi, nimezoea kufanya kazi usiku.

Akifafanua anasema kwamba akiwa hana kazi za uDJ basi usiku huo anajikuta akitazama movie usiku kucha au kufanya kaiz nyingine aliyonayo.

“Ndio maana hata mahojiano nanyi nimefanya saa sita usiku, nimejibu maswali yenu usiku kwa sababu sikuwa kazini siku hiyo na sikuwa na usingizi,’’ anasema DJ huyo ambaye pia ni mwajiriwa wa Clouds Radio

Aliingiaje kwenye uDJ.

DJ Sinyorrita anasema tangu akiwa shule alikuwa akipenda kusikiliza muziki na kuvutiwa na kazi ya DJ na ilivyofika mwaka 2012 aliwashirikisha baadhi ya watu wake wa karibu na kuwaeleza kuwa angependa kujifunza kazi hiyo.

“Kwa kuwa nilikuwa najuana na baadhi ya watu walinipeleka ukumbi wa disco Maisha Club na kunikutanisha na DJ Park ambaye alikuwa akipiga muziki pale na kuanza kunifundisha.

“Ili kupishana na ratiba zao nilikuwa nikienda kujifunza saa kumi jioni na inapofika usiku disco likianza naenda kukaa pembeni kuangalia namna wanavyofanya,” anasema.

Anasema alijifunza kazi hiyo kwa mwaka mmoja na kuelewa vema. “DJ Park aliniunganisha na kundi lao la MaDj waliokuwa wakipiga muziki katika maeneo mbalimbali.

“Nakumbuka kazi ya kwanza kufanya ilikuwa Coco Beach na baadaye nikapata uzoefu na kufanya Masai Club Kinondoni,” anasema.

Hata hivyo anasema kutokana na uchache wa MaDJ wa kike, watu walikuwa wanamchukulia ndivyo sivyo, wengine walikuwa wakimshangaa, wengine wakimchukulia kuwa ni muhuni.

“Awali macho ya watu yalinipa shida, nilikuwa naona aibu, lakini kadri siku zilivyozidi kwenda nilijikuta nazoea,” anasema.

Mwaka 2014 akiwa anaendelea kufanya kazi hiyo uongozi wa Samaki Samaki Mlimani City ulivutiwa naye na kumchukua ambapo alikuwa akipiga muziki kila Jumamosi.

Anasema akiwa hapo alikuwa halipwi vizuri lakini fedha alizokuwa akitunzwa na mashabiki wa muziki, zilikuwa zikimuweka mjini na pia alikuwa akipata ‘connection’ za kazi nyingine.

“Nakumbuka nikiwa hapo nilikutana na watu wanajiita Just be Paid, ambao walikuwa wakiandaa sherehe ya watu kukutana pamoja kila mwisho wa mwezi, hao ndio walikuwa watu wa kwanza kunilipa vizuri, anasema Sinyorrita bila kutaja kiwango alichokuwa akilipwa kwa madai kuwa ni siri yake.

Akiwa hapo mwaka 2015 akaonwa na uongozi wa kituo cha redio cha East Africa ambao walimpigia simu na kumtaka aende kwa ajili ya kufanyiwa usaili wa kazi ambapo alipitishwa na kuajiriwa.

Kutokana na kubanwa na mkataba wa ajira East Africa ikabidi aachane na Samaki Samaki baada ya kufanya kazi miezi sita.

“Naona safari yangu ya mafanikio ilikuwa imeshika kasi. Mwaka 2016, Clouds walinipigia simu wakitaka kufanya kazi nami.

“Kama kijana nilikuwa nina wazo la kufanya kazi mahali tofauti ili nijifunze lakini pia nisikilizwe na watu wengi zaidi, nilipoitwa sikujivunga nilifanyiwa taratibu na kujiunga nao na nipo hadi sasa”anasema.

Changamoto

Katika ufanyaji kazi huo anasema amejikuta akiathirika katika suala zima la kulala usiku.

“Yaani hata kama siku sina kazi ya usiku najikuta tu nakosa usingizi na ikitokea mchana nafanya kazi basi naifanya huku macho yakiwa mazito ila kwa kuwa ni kazi inabidi nipambane,” anasema.

Changamoto nyingine ni watu kumchukulia muhuni, baadhi ya wanaume hutumia fursa hiyo kumtongoza na kuona rahisi kumpata bila kujua yupo kazini. Anasema hii humtokea wakati mwingine watu kumuomba namba za simu wakimwambia wanataka kufanya naye kazi, lakini anapofika kufanya nao kikao wanaanza kumtongoza.

Mafanikio

Anasema kupitia kazi hiyo, anamudu pango la nyumba, amenunua kiwanja, anamiliki gari na kuendesha maisha yake ya kila siku.

Pia amekuwa akipata kazi ndani na nje ya nchi zinazomuwezesha kupata hela na nyingine kukutana na watu tofauti. “Nimewahi kupata mialiko Nairobi mara mbili, Malaysia mara mbili, Oman, Dubai na Rwanda nimeshindwa kwenda kutokana na mlipuko wa corona,’’ anasema.

Pia kuna wakati DJ Sinyorrita hufanya kazi bure hasa akigundua atapata connection ya kazi nyingine, kwake ni bora kuliko kupata fedha.

DJ Sinyorrita anawaasa watu kuthamini kazi ya MaDJ kwa kuwalipa vizuri, kwani ni kazi kama nyingine.

“Jamii pia itambue mabadiliko ya teknolojia na ya dunia kwa ujumla yameondoa mipaka ya kazi za wanaume na wanawake, wawachukulie maDJ wa kike kama wanavyowachukulia polisi, madaktari, manesi, badala ya kuwapachika jina la uhuni”anasema.