Harusi ya MC Pilipili kufanyika mikoa mitano

Tuesday March 26 2019

 

By Nasra Abdallah

Siku chache baada ya mshehereshaji Emmanuel Mathias ‘MC Pilipili’, kueleza harusi yake itakuwa na kiingilio kwa waalikwa, amekuja na jambo lingine jipya akitangaza ufanyikaji wa sherehe hiyo.

Akizungumza na Mwananchi, MC Pilipili, alisema kutokana na watu wengi kutaka kuishuhudia harusi hiyo, yeye na kamati zake wamepanga itafanyika katika mikoa mitano nchini.

Aliitaja mikoa hiyo ni Mwanza, Geita, Arusha, Dodoma na Dar es Salaam, huku akieleza huenda baadaye ikaongezeka zaidi.

“Hii ni sherehe ya MC wa Taifa, hivyo lazima ifanyike kitaifa, mikoa hiyo ni michache tu ambayo imeshapitishwa na kamati katika vikao vinavyoendelea maeneo hayo, huenda ikawa mingi zaidi kadri siku zinavyokwenda, nitawataarifu,” alisema.

Mshereshaji huyo, Januari mwaka huu aliibua gumzo mitandaoni baada ya kuonekana akilia wakati wa hafla ya kumvisha pete mchumba wake , Philomena Thadey. (Nasra Abdallah).

Advertisement