Mondi anapomuibua Kiba kwa pepo la kisulisuli

Saturday November 2 2019

Harmonize,Diamond ,Msanii wa muziki wa Bongo Fleva,mwananchi habari, gazeti la mwananchi,Naseeb Abdul,

 

By Dk Levy

Hawa ni madogo tu, hasira za maisha walihamishia kwenye muziki. Kuna madogo kibao wa Kariakoo wamefia nje ya nchi au magerezani kwa kubebeshwa dawa za kulevya. Na kuna madogo wengi sana wameuawa kwa wizi au kwa matumizi ya dawa za kulevya huko Tandale. Wote walitaka kuishi maisha wanayoishi Kiba na Mondi hivi sasa.

Ni Mondi na Kiba tena. Baada kimya kirefu wamerejea tena na yaleyale kwa mtindo mwingine. Wanachosha lakini ndo mashine za kutengeneza habari. Ni mastaa haswa na wanapendwa. Na zaidi wana watu wengi nyuma yao. Mimi nikiwapuuza kuna mamilioni ya watu wataacha kazi zao na kuwajadili. Mimi ni nani sasa hata nisiwajadili?

Kuna mmoja makuzi yake ya Kariakoo (Uswahilini) na kuna mwingine makuzi ya Tandale (Uswahilini) huwaambii kitu maana wanayajua maisha ya kitaa kindakindaki. Wanapiga pesa nyingi kupitia muziki na hawajaacha kudumisha mila ya Uswahili. Pesa ipo, majina yako na Uswahili upo vilevile. Hawa ni alama sahihi ya watoto wa Kiswahili.

Wakati ule kosa lilikuwa pini la ‘Zilipendwa’. Mondi na masela wake wa WCB walilitoa kwa kushtukiza. Bila kuumauma maneno ni kwamba lengo lilikuwa kuuzima upepo wa ngoma mpya ya Kiba ile ‘Seduce Me’. Lilikuwa kosa kubwa kwani huruma ya watu ilipindua meza Mondi akaonekana kituko mwenye roho mbaya.

‘Seduce Me’ haukuwa wimbo wa ajabu kati ya ngoma kibao za Kiba. Lakini michongo ya Dai kutaka kufunika ikafanya wimbo uwe mkubwa umma ukawa upande wa Kiba. Akaonekana kama mnyonge anayeonewa. Kilichotokea ni wimbo mzuri wa ‘Zilipendwa’, wa WCB kuonekana wa kawaida mno. Hasira za watu.

Hata ujio mpya wa Kiba ulikuwa namna hii. Kabla ya kuachia ngoma ya ‘Mwana’ ambayo haikufikia kiwango cha ‘Dushelele’ alianza kwa ‘intavyuu’ na mwanadada mmoja mitandaoni. Huko ndiko jina la King lilianza kumea baada ya kudai anafuta kiti chake cha ufalme na akikalie yeye mwenyewe.

Advertisement

Katika maelezo yake pia alitoa madai ya kufutwa kwa sauti yake kwenye moja ya ngoma za Mondi. Alijibu hivi kutokana na mahojiano hayo ambayo yalikuwa sahihi kwa wakati ule. Ni wakati ambao watu walitaka kuondoa ‘Udiamond’ kwenye ‘gemu’. Hapo hakuna Belle 9 wala Rich Mavoko. Wote hao alishindanishwa nao kabla ya ujio Kiba.

Kiba akaonekana mtu sahihi wa kumfunika. Ushindani wao ndipo uliposhika kasi na kuotesha timu ambazo hazitambuliki Fifa wala Tff. Hili narudia mara nyingi kusema, Wabongo hawapendi mtu mmoja awe juu kila siku watatamani au kulazimisha apatikane wa kukushusha au uporomoke tu. Hata kama mtu yuko vizuri zaidi.

Sugu na Profesa Jay busara zao kama wasanii ziliwasaidia kuendelea kuheshimiana. Wakati Jay anaanza kukamata ‘laini’ miaka ya 2000 wapo walioamini kama mtu sahihi wa kutingisha utawala wa Sugu. Kwa sababu Sugu alisikika peke yake muda mrefu kuanzia zinduzi za albamu mpaka tuzo. Usisahau ‘bifu’ lake na wadau wa muziki.

Hizi hisia zipo kwenye gemu la Bongofleva kwamba Joh Makini alitumika kumpoteza Fid Q hizi hisia zipo au Chid Benz alijengwa kumpoteza Jay. Unaishia kucheka kuona The Heavy Weight Mc na Chid Benz wapi na wapi? Lakini ndo Siasa kwenye ‘gemu’. Hata waliopata tuzo walionekana kupewa ili kuumiza mwingine.

Upuuzi huu uliendelea kuwepo mpaka hapa juzi eti Billnas aliletwa ili kumfunika marehemu Godzilla. Sasa mtu unajiuliza Zilla alifikia daraja gani mpaka akatafutiwa mpinzani? Hili ‘gemu’ lina pesa nyingi lakini kuna eneo wasanii hukwama ili kuzifikia nyingi mbele zaidi. Ni kama kuanzisha bendi ili kuipoteza bendi.

Mr Nice katika muziki wake hakuwahi kuwa na mpinzani akaundwa Dudubaya ambaye hawakufanana kuanzia muziki, mwonekano, tabia, sauti na kila kitu. Lakini akawa mpinzani wake mkuu kwenye akili za Wabongo wengi. Hata mtoko wa H Baba ni kutafuta mpinzani halisi wa Nice. Hizi siasa zimeua sana nyoyo za wanamuziki wengi.

Hili halijaja bahati mbaya lipo kwenye fikra za wadau na wanamuziki wenyewe. ‘Andagraundi’ anapotaka kutoka hawazi kuendeleza sanaa kwa ujumla wake. Wanapotoka huwaza na kutamani kuwa kama fulani na waliotoka tayari wanawaza kuwa wao wenyewe kileleni. Hawataki kusogelewa. Tatizo lingine ni wasimamizi wa wasanii wengi wao ndiyo wamiliki wa vituo vya redio au runinga kama siyo watendaji kwenye vituo hivi. Hawataki kuweka uwanja huru kwa kila msanii. Wanataka wasanii wao kwanza kwenye kila kitu. Na tatizo meneja wa msanii, redio, runinga ndiye huyohuyo mwendeshaji wa matamasha.

Ukiwa nje ya mikono yake hupati nafasi runingani. Huna chako redioni na huwezi kupewa nafasi ya kushiriki tamasha kubwa. Umiliki wa vyombo vya habari hutumika kama fimbo. Sioni Harmonize akisikika Wasafi Fm, Wasafi Tv wala Wasafi Festival. Ikiwa ndivyo sivyo basi yatakuwa maajabu. Hii hulka tunarithi kizazi na kizazi.

Hii ndiyo sababu ya Mondi aliulizwa kama Kiba na Harmo watakuwepo Wasafi Festival. Kwa sababu wasanii wengi kukosa michongo ya show na ‘airtime’ wanapotofautiana na mabosi wa media nyingi. Licha ya Mondi kudai Kiba kapelekewa ombi la kushiriki. TeamKiba na Kiba mwenyewe wanaamini ni unafiki.

Majibu ya Mondi hayakuwa mabaya kiasi cha Kiba kumshambulia vile. Lakini kama utakuwa mfuatiliaji wa mitoko ya Kiba na Mondi siku za karibuni hutoshangaa. Mondi anaweza kuwa kamtaja Kiba kusudi kwa sababu anajua hili lingetokea. Na Kiba anaweza kuwa kajibu kusudi kwa faida yake. Mondi anafahamu akimtaja Kiba kwenye lolote hugeuka ‘topiki’. Na tamasha kama hili kuongelewa kwanamna hii ni matangazo makubwa zaidi. Na Kiba huenda kajibu makusudi ili atoe ngoma mpya.

Kiba na uongozi wake wanajua hizi kelele humsaidia zaidi akiwa na mtoko. Kuna ujio wa ngoma mpya ya Kiba bia shaka.

Majibu ya Kiba baada ya kauli ya Mondi hata hayaendani. Ni kama Kiba au uongozi wake wameamua kutoka na upepo huu wa kisulisuli ili kuachia ngoma jipya. Wamepata sababu ya mchomoko baada ya ngoma kadhaa hapo kati kuja na kuondoka kama upepo. Hapa Mondi anaweza kuwa katoa boko lingine.

Huu upepo wa kisulisuli unaweza kuwa mzuri kwa ujio mpya wa Kiba. Hasa ngoma akiipa jina la neno aliloandika kwa herufi kubwa mtandaoni. Lakini akumbuke kuwa watu hudanganywa kwa wingi mara moja. Huwezi kuwadanganya kwa wingi uleule kila mara. Si wakati wa kusubiri huruma za watu au drama za madem.

Mondi ngoma zake hutoa kwa drama za madem. Kiba naye anasubiri hutoa baada ya majibizano na Mondi. Lakini tukifuatilia ngoma kama ile ya ‘Chibonge’ au ‘Uno’ la Harmo. Mbona zinakimbiza mitaani bila drama za bifu na madem? Leo 50 Cent na Jah Rule wote wametoweka, kwa ‘gemu’ la drama badala ya kazi bora.

Leo hii ukisikia Mondi kaachana na Natasha. Utasikia hana lolote huyo anataka kutoa wimbo mpya huyo. Mashabiki wameshajua kuwa akimfanyia tukio dem wake, basi ujue ni kiki ya ujio wa ngoma mpya. Kiba anataka kuelekea huko katika kuamini kiki na siyo muziki mzuri. Katikati ya hawa jamaa wawili kuna tundu. Sijui hili tundu nani atalitumia ili kuipasua hii miamba miwili. Lakini kwa namna ambavyo vichwa vya watu vilivyo na mambo mengi inawezekana. Kama juzi neno lililokamata lilikuwa ni “Mabaharia” leo hii ni “Upepo wa Kisulisuli”. Ni kwamba vichwa vya watu vinanasa na kusahau haraka jambo hivi sasa.

Wakati unamtazama Mondi na Kiba. Elewa kuwa ni madogo waliokulia maeneo ambayo vijana wengi hawapo hai au uraiani. Ni mitaa inayozalisha kundi la vijana wenye tamaa ya maisha aliyonayo hii leo Mondi na Kiba. Mkwanja mrefu bila kutegemea elimu. Wanaishia kukaba, kujidunga, kubebeshwa nyunga na kufia magerezani.

Unapoona Mondi na Kiba wamesimama pale mtaani wameacha vichaa kibao.

Ambao wamekuwa vichaa kwa kushindwa kufikia pale walipo. Acha pesa ziwatie wazimu, safari ya kuzisaka kwa kutokea Uswahilini huwa ngumu sana. Mungu awape nini? Waache wadumishe mila ya Uswahilini kwa kuishi Kiswahili. Acha wasutane.

Advertisement